• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:55 AM
ANA KWA ANA: Ngoma tata ila zazidi kutetemesha tasnia

ANA KWA ANA: Ngoma tata ila zazidi kutetemesha tasnia

Na PAULINE ONGAJI

HII wikendi watakuwa miongoni mwa wasanii watakaomfungulia jukwaa kigogo wa AfroBeat Femi Kuti katika makala ya 26 ya Koroga Festival.

Hii ni ishara kuwa muziki wao unazidi kukubalika licha ya video zao kuonekana waziwazi kuendekeza masuala ya ngono kutokana ‘video vixens’ wanaonengua kwa staili ya kuchochea mihemko ya mahaba.

Ni suala ambalo limewapa Boniface ‘Swat’ Mwangi, Peter ‘Zilla’ Njau, Leeroy ‘Seska’ Miwa na Thomas ‘Rekles’ McDonald, wanaojumuisha kikundi cha Ethic, umaarufu mkubwa hata ingawa wamekuwa ulingoni kwa mwaka mmoja pekee.

Kufikia sasa, kikundi hiki chenye chimbuko lake mtaani Umoja, jijini Nairobi, kinajivunia vibao kadhaa ikiwa ni pamoja na Lamba Lolo, Pandana, Instagram,Saba, New Position na cha hivi punde Figa ambacho tayari kina ‘views’ zaidi ya milioni moja kwenye YouTube.

Safu hii ilipata fursa ya kuketi kijiweni nao na hivi ndivyo mambo yalikuwa.

Kikundi hiki kilibuniwa mwaka jana tu, mlikutana vipi?

ETHIC: Tulikuwa tumewekeza pamoja kwenye duka la video mtaani Umoja. Biashara hii ndiyo iliyotufungua macho na kutusaidia kugundua penzi letu katika muziki. Mbeleni kila mmoja alikuwa akiimba solo ila tulipogundua kwamba sote tuna vipaji vya vipekee, tuliamua kushirikiana.

Sio siri kwamba jumbe na video zenu ni chafu na zimepotoka kimaadili. Je, mwasaka kiki nini?

ETHIC: La hasha! Hatufanyi kazi zetu ili kupata kiki. Tunaamini kwamba tunachoimba kinaakisi sura halisi ya jamii yetu ya sasa na ndio sababu himaya yetu yakua kwa kasi.

Je, hizi video zinasawiri maisha yenu halisi?

ETHIC: La! Hiyo ni kazi tu. Pindi kamera zinapozimwa, sisi hurejelea maisha yetu kama vijana wa kawaida mtaani.

‘Video vixens’ wenu wanoma sana katika kunengua. Je, mnawapata wapi?

ETHIC: Kuna baadhi yao ambao hutujia wenyewe, ilhali wakati mwingine sisi hujitafutia mabinti watakaohusishwa kwenye video zetu.

Je, kuna nyakati ambapo mnakosolewa kwa kazi zenu?

ETHIC: Ni rahisi sana kukosolewa unapofanya kitu kizuri. Naam, tumekosolewa sana na baadhi ya watu hasa wa kizazi cha zamani. Lakini pole pole hata wao wameanza kukubali muziki wetu. Watakosaje na hata watoto wao wanausikiza na hata kuimba?Hata hivyo wasitie shaka kwani hivi karibuni tutawapa kitu cha kudondosa nyoyo zao.

Je, kazi zenu “tata” haziwanyimi nafasi za kufanya kolabo na wenzenu?

ETHIC: La hasha! Kinyume na dhana hiyo, orodha ya wanamuziki wanaosaka kolabo nasi ni ndefu ajabu.

Miezi mitatu iliyopita kulisambaa video mtandaoni iliyoonekana kumuonyesha Swat akipigwa na kikundi cha watu. Baadaye kulienea uvumi kwamba hii ilikuwa baada ya yeye pamoja na wenzake kufumaniwa na polisi wakivuta bangi. Hebu tuweke wazi?

ETHIC: Suala hilo la bangi sio kweli kabisa. Ukweli ni kwamba Swat aliingia jengo fulani na hivyo akachukuliwa kimakosa kuwa mwizi. Kando na hayo, iwapo kwa kweli angekuwa mwizi, basi angekuwa ashafikishwa mahakamani na kufunguliwa mashtaka.

Nini kilichosababisha kuvunjika kwa uhusiano kati yenu na meneja wenu wa zamani, Mwakitele?

ETHIC: Hamna kikubwa. Tulikuwa tunataka mambo tofauti kuhusu muziki wetu. Zaidi ya yote hatujawahi kuwa maadui.

Mnafahamu kuwa kumekuwa na uvumi kuhusu kuwepo kwa kesi mahakamani baina yenu na meneja huyu wenu wa zamani, inaendeleaje?

ETHIC: Hakuna kesi yoyote mahakamani kati yetu naye. Mwakitele anasalia kuwa mmojawapo wa washirika wetu wakuu.

You can share this post!

JANDONI: Uganda katika mizani raundi ya 16-bora ikianza

Ruto afinywa

adminleo