Habari

Sababu za kuteuliwa miswada inayopendekeza wabunge wateuliwa kutoka bungeni

July 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na CHARLES WASONGA

MPANGO wa kuwawezesha wabunge kuteuliwa kuwa mawaziri ulipigwa jeki bungeni baada ya afisi maalumu ya kamati ya bunge kuhusu bajeti kuunga mkono.

Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wa imeidhinisha miswada miwili inayolenga kuifanyia Katiba marekebisho ili kuondoa hitaji kwamba mawaziri hawapaswi kuwa wabunge.

Wabunge Vincent Kimose (Mugirango Magharibi) na William Kamket (Tiaty) wamedhamini miswada miwili tofauti ambayo iliidhinishwa na kamati hiyo ya bajeti Alhamisi na kutoa nafasi ya kuwasilishwa kwayo rasmi bungeni.

Katika mswada wake, Bw Kimose anapania kukifanyia marekebisho kipengee 152 (3) cha Katiba kwa kuondoa maneno, “Waziri hapaswi kuwa mbunge”.

Aidha, mswada huo upendekeza kuwa idadi ya mawaziri ipungunzwe kutoka 22 hadi 14 kwa kuifanyia marekebisho kipengee cha 152 (1) cha Katiba kinachosema kuwa idadi ya mawaziri haipasi kuwa chini ya 14 au kuzidi 22.

“Lengo kuu la mswada huu ni kupunguza mzigo wa gharama ya mishahara ya watumishi wa umma. Vilevile, unalenga kuhakikisha kuwa wabunge wanapata fursa ya kuwauliza mawaziri maswali kuhusu masuala yanayohusu maeneobunge hao,” Bw Kemosi akasema.

Afisi inayotoa ushauri kuhusu masuala ya fedha bungeni (PBO) pia iliidhinisha marekebisho yanayopendekezwa na mswada huo lakini ikasema sharti yaidhinishwe katika kura ya maamuzi.

Hii, kulingana na PBO, ni kwa sababu marekebisho hayo yanaathiri majukumu ya bunge.

“Pendekezo la kuteua mawaziri kutoka bunge litawaokoa Wakenya Sh223 milioni kila mwaka. Hata hivyo, kura ya maamuzi itagharimu Sh15 bilioni, gharama ya mara moja,” inasema ripoti ya afisi ya PBO.

Mswada mwingine ambao uliidhinishwa na Kamati ya Bw Ichung’wa ni ule wa Bw Kamket ambao pia unapendekeza kuwa mawaziri wateuliwe kutoka miongoni mwa wabunge.

Mamlaka

Vilevile, mbunge huyo wa chama cha Kanu anapendekeza kubuniwe wadhifa wa Waziri Mkuu mwenye mamlaka ambaye ataongoza serikali na Rais asiwe mwenye mamlaka.

Pia Bw Kamket anapendekeza kubuniwa upya kwa wadhifa wa Kiongozi Rasmi wa Upinzani.

Miswada hiyo miwili hata hivyo inapaswa kupitishwa na thuluthi mbili ya jumla ya wabunge; ambayo ni wabunge 233, kwa sababu miswada hiyo inalenga kubadili mfumo wa utawala kutoka ule ya urais hadi utawala wa mseto (wa mfumo wa ubunge na urais).

Chini ya mfumo wa utawala wa mseto, wapiga kua huchagua Rais moja kwa moja kuwa kiongozi wa serikali na wabunge miongoni mwa wale ambao mawaziri watateuliwa.

Bw Ichung’wa alisema kamati yake imepokea ushauri kutoka kwa afisi ya bajeti bunge na inashauriana na Hazina ya Kitaifa kuhusu masuala ya kifedha yatakayoibuliwa na miswada hiyo.

“Wajibu wa kamati yangu ni kuchunguza miswada yenye mahitaji ya kifedha. Hatuhusiki na masuala ya kisheria kuhusu miswada,” akaeleza Mbunge huyo wa Kikuyu.

Kulingana na PBO, majukumu ya bunge yako kwenye vipengele vinavyohitajika kubadilishwa kupitia kura ya maamuzi.

Kwa hivyo, uchanganuzi unabaini kuwa mtindo wa kuteua mawaziri kutoka miongoni mwa wabungu utapunguza idadi ya maafisa wa serikali.

“Kwa hivyo, hatua hii itapunguza gharama kama vile za usafiri na ulinzi japo kutahitaji kura ya maamuzi ikakayogharimu Sh15 bilioni. Mbunge ambaye atateuliwa kuwa waziri atapokea marupurupu zaidi ya majukumu ya Sh400,000,” inasema taarifa ya ushauri kutoka PBO.

Gharama ya utekelezaji wa miswada hiyo itakuwa Sh15 bilioni, gharama mara moja huku ikiokoa Sh223.7 milioni kila mwaka.

Wakati huu Waziri hupokea Sh924,000 kama mshahara na marupurupu, kila mwezi. Na serikali kutumia jumla ya Sh243.9 milioni kila mwaka kugharamia mishahara na marupurupu ya mawaziri.

Na ikiwa mawaziri wateuliwa kutoka bunge gharama hiyo itapungua hadi Sh105.6 milioni.

Kuhusu malipo ya pensheni, ripoti ya PBO inasema kuwa uteuzi wa mawaziri kutoka bungeni utasaidia serikali kuokoa Sh85.4 milioni ikilinganishwa na hali ya sasa ambapo mawaziri sio wabunge.

Kulingana na afisi hiyo, madhara ya uteuzi wa mawaziri kutoka bunge ni kwamba sehemu ya serikali itakuwa bungeni na hivyo utengano wa mamlaka unatakiwa kisheria utakosekana.

Na endapo mbunge atateuliwa Waziri hali hiyo itaathiri, kwa kiwango fulani, huduma yake kwa eneo bunge lake.