Makala

MWANAMKE MWELEDI: Ni mwanga kwa watoto wa kike

July 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na KEYB

WAMAASAI wanajulikana ulimwenguni kote kutokana na utamaduni wao thabiti, vilevile kama mojawapo ya jamii ambazo zimefanikiwa kuhifadhi mila na desturi zao za kale.

Hata hivyo, baadhi ya tamaduni zao kama vile ukeketaji na ndoa za mapema zimekuwa zikirudisha maendeleo ya jamii hii nyuma.

Ni suala ambalo lilimsukuma Kakenya Ntaiya kuingilia kati na kutaka kuwanasua watoto wasichana kutokana na baadhi ya tamaduni hizi.

Bi Ntaiya amechangia pakubwa katika shughuli za kuelimisha watoto wasichana kutoka jamii yake. Ni kazi ambayo amekuwa akifanya kwa zaidi ya mwongo mmoja sasa, kupitia kituo cha Kakenya Center for Excellence, shule aliyoanzisha mwaka wa 2008.

Mojawapo ya masuala yanayofanya shule hii kuwa maalum ni masharti yaliyowekewa wanaotaka kujiunga nayo. Kwanza, wasichana hawa hawapaswi kuwa wamekeketwa, na pili, kunapaswa kuwa na hakikisho kwamba hawataozwa au kuolewa mapema.

Shule hii ilifunguliwa rasmi Mei 2009 huku ikiwa na wanafunzi 32 pekee. Na matunda yake tayari yanashuhudiwa kwani katika kipindi hiki, asilimia 100 ya wanafunzi wake wa zamani wamejiunga na shule ya upili.

Mbali na hayo, mwaka wa 2011, shule hii ilizindua mradi wa afya na uongozi kwa minajili ya kukabiliana na tamaduni zinazorejesha watu nyuma kama vile ukeketaji na ndoa za kulazimishwa.

Aidha, shule hii ina mradi mwingine kwa jina Network for Excellence unaohakikisha kwamba wanafunzi wanasalia shuleni, kando na kuwasaidia kufuata na kutimiza ndoto zao baada ya kuondoka shuleni.

Ari yake ya kuanzisha mradi huu ilitokana na changamoto zinazokumba wasichana wengi kutoka jamii ya Wamaasai.

Hizi ni baadhi ya changamoto alizokumbana nazo alipokuwa akikua kabla ya kupata elimu. Akiwa na miaka mitano pekee alichumbiwa rasmi na mvulana wa miaka sita.

Aidha kama kifungua mimba katika familia ya watoto wanane, alikumbwa na majukumu mengi akiwa bado mchanga kiumri, ikiwa ni pamoja na kuwashughulikia nduguze wadogo, kulima na kufanya kazi katika mashamba ya miwa.

Babake ambaye alikuwa afisa wa polisi na ambaye alikuwa akifanya kazi mbali kidogo, alimuachia jukumu la kumsaidia mamake kushughulikia wadogo zake.

Kwa hivyo ili kukamilisha elimu, aliingia katika maafikiano na babake.

Akubali kukeketwa

Alikubali kukeketwa ili kwa upande mwingine aruhusiwe kuendelea na kukamilisha masomo yake.

Ni suala lililozaa matunda kwani aliweza kukamilisha shule ya upili na hata kupata nafasi ya kujiunga na chuo kikuu kimoja nchini Amerika.

Hata hivyo masaibu yake hayakuwa yamekwisha. Ndoto hiyo ilikatizwa kwani familia yake haingeweza kumfadhili kuendelea na masomo hasa nchini Amerika.

Hii ni hasa ikizingatiwa kwamba babake alikuwa mgonjwa kiasi cha kupooza na kulazwa hospitalini.

Kutokana na janga hili, familia yake ilizamika kuuza mali ili kulipa bili ya hospitali.

Lakini matatizo hayo hayakuzima kiu yake ya kujiimarisha kielimu. Ili kuendelea na masomo, alikata kauli na kumwendea kiongozi wa kijiji ambaye alikuwa na usemi mkubwa.

Kiongozi huyu aliweza kushawishi wanakiji kumchangia pesa za kufadhili masomo yake nchini Amerika.

Kwa sasa Bi Ntaiya anaendelea kusimama imara na ananuia kwamba shule yake itazidi kuendesha shughuli hizi katika siku zijazo na hata kukuza viongozi wanawake watakaobadilisha ulimwengu.