Malkia yatua nchini Misri kwa mpepetano wa Bara Afrika
Na GEOFFREY ANENE
WASHIKILIZI wa mataji mengi ya Kombe la Voliboli ya wanawake barani Afrika, Kenya, wametua jijini Cairo nchini Misri kwa makala ya mwaka 2019.
Timu hiyo almaarufu Malkia Strikers, ambayo inajivunia kushinda mataji ya mwaka 1991-1997, 2005-2006 na 2011-2015, iliondoka jijini Nairobi mapema Ijumaa.
Nchini Misri, warembo hao wa kocha Shailen Ramdoo watakuwa na kibarua kigumu cha kurejesha taji ambalo Kenya ilipoteza mwaka 2017 baada ya kucharazwa na Cameroon kwa seti 3-0 (25-22, 25-19,29-27).
Wakenya watapigania taji dhidi ya Misri, Tunisia, Ghana, Libya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Cameroon, Morocco, Nigeria, Algeria, Botswana, Rwanda na Chad.
Baadhi ya timu zilizo na uzoefu mwingi katika mashindano haya zinazotarajiwa kuwa wapinzani wakali kwa Kenya ni Misri na Tunisia, ambao wote wameshinda mataji matatu kila mmoja, washindi wa mwaka 2009 Algeria na mabingwa watetezi Cameroon.
Timu ya Rwanda pamoja na Nigeria na Botswana zimekuwa zikiimarika kwa hivyo haziwezi kudharauliwa.
Kenya imekuwa ikijiandalia mashindano haya tangu mwezi Mei katika ukumbi wa kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi.
Ziara ya Malkis Strikers nchini Misri ni mwanzo wa shughuli nyingi itakuwa nazo kwa miezi michache ijayo kwa sababu pia itashiriki mashindano ya kufuzu kushiriki Olimpiki mwaka 2020 itakayofanyika nchini Italia mnamo Agosti 2-4, 2019, michezo ya African Games nchini Morocco mnamo Agosti 19-31 na Kombe la Dunia nchini Japan mwezi Septemba 14-29.
Kikosi cha Malkia Strikers:
Maseta – Jane Wacu, Janet Wanja;
Malibero – Agrippina Kundu, Elizabeth Wanyama;
Wachezaji wa kati – Triza Atuka, Brackcides Agala, Edith Wisa, Gladys Ekaru;
Washambuliaji wa pembeni kushoto – Mercy Moim, Sharon Chepchumba, Leonida Kasaya, Noel Murambi;
Washambuliaji wa pembeni kulia – Violet Makuto, Immaculate Chemtai.