Habari

TUKUTANE KASARANI: Everton yatua jijini Nairobi tayari kukabiliana na Kariobangi Sharks

July 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

KIKOSI cha Everton FC kitakachopambana na Kariobangi Sharks katika mechi yake ya kwanza ya kujiandalia msimu 2019-2020, kimetua jijini Nairobi tayari kwa mchuano utakaosakatwa uwanjani Kasarani hapo Jumapili.

Baadhi ya majina makubwa katika kikosi hicho cha kocha Marco Silva ni mchezaji wa zamani wa Manchester United Morgan Schneiderlin, nyota wa zamani wa Arsenal Theo Walcott, mchezaji wa zamani wa Barcelona Andre Gomes na Leighton Baines.

Silva hana wachezaji Jordan Pickford, Seamus Coleman, Lucas Digne, Gylfi Sigurdsson na Michael Keane katika kikosi chake. Kulingana na gazeti la Liverpool Echo, watano hawa wataanza mazoezi uwanjani Finch Farm mnamo Julai 8.

Vilevile, mshambuliaji chipukizi Kieran Phillips, ambaye alisaini kandarasi ya mwaka mmoja Ijumaa, hayuko kikosini sawa na nyota wa Uturuki Cenk Tosun, Mbrazil Richarlison, Yannick Bolasie (DR Congo), Yerry Mina (Colombia), Mbrazil Bernard, Mfaransa Kurt Zouma na Idrissa Gana Gueye (Senegal).

Tosun bado anaendelea kupona jeraha nao Richarlison na Bolasie wanawakilisha mataifa yao katika Kombe la Amerika Kusini (Copa America) na Kombe la Afrika (AFCON) nchini Brazil na Misri, mtawalia.

Mina na timu yake ya Colombia ilibanduliwa nje ya Copa America katika robo-fainali, lakini anatarajiwa kupewa likizo ya siku kadhaa kabla ya kujiunga na Everton kwa mechi zaidi za kujipiga msasa. Gueye pia yuko nchini Misri kwa AFCON.

Dominic Calvert-Lewin na Kieran Dowell pia hawapo baada ya kujumuishwa katika timu ya taifa ya Uingereza ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 21.

Dowell alichangia bao moja na Wayne Rooney lingine Everton ikichapa mabingwa wa makala ya kwanza ya SportPesa Super Cup Gor Mahia mwaka 2017 jijini Dar es Salaam.

Mwaka 2018, Everton ilialika washindi wa makala ya pili ya SportPesa Super Cup Gor uwanjani Goodison Park nchini Uingereza kwa mchuano mwingine wa kujipima nguvu. Ilipepeta mabingwa hao wa Kenya 4-0 kupitia wachezaji Ademola Lookman, Dowell, Nathan Broadhead na Oumar Niasse.

Mabingwa hawa mara tano wa Kombe la FA watalimana na Sion ya Uswizi (Julai 14), Monaco kutoka nchini Ufaransa (Julai 19), Wigan ya Uingereza (Julai 24) na Mainz kutoka Ujerumani na Sevilla kutoka nchini Uhispania (Julai 27) na Werder Bremen kutoka Ujerumani (Agosti 3) katika mechi zingine za kirafiki baada ya kupimana nguvu dhidi ya Sharks, ambao ni washindi wa soka ya SportPesa Super Cup.

Vijana wa Marco Silva wameratibiwa kurejea nchini Uingereza baada tu ya kumenyana na Sharks kabla ya kuelekea nchini Uswizi kwa mechi zaidi za kirafiki na maandalizi ya msimu mpya.

Kikosi cha Everton jijini Nairobi 2019: Maarten Stekelenburg, Jonas Lossl, Mason Holgate, Lewis Gibson, Morgan Schneiderlin, Dennis Adeniran, Tom Davies, Theo Walcott, Ademola Lookman, Leighton Baines, Andre Gomes, Oumar Niasse, Ryan Astley, Callum Connolly, Morgan Feeney, Antonee Robinson, Beni Baningime, Joe Williams, Nathan Broadhead, Fraser Hornby, Josh Bowler na Nathangelo Markelo.

Kikosi cha Everton jijini Dar es Salaam 2017: Maarten Stekelenburg, Jonjoe Kenny, Ashley Williams, Phil Jagielka, Callum Connolly, Morgan Schneiderlin, Aaron Lennon, Ademola Lookman, James McCarthy, Davy Klaassen, Wayne Rooney, Mateusz Hewelt, Matthew Pennington, Leighton Baines, Muhamed Besic, Michael Keane, Kevin Mirallas, Dominic Calvert-Lewin, Gareth Barry, Idrissa Gana Gueye, Kieran Dowell.