Michezo

Cheruiyot afuta rekodi ya miaka 18 ya mbio za mita 1,500 Lausanne

July 6th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

TIMOTHY Cheruiyot, Wycliffe Kinyamal na Nelly Jepkosgei waliibuka washindi wa mbio za mita 1,500 (wanaume), mita 800 (wanaume) na mita 800 (wanawake) kwenye duru ya nane ya Riadha za Diamond League mjini Lausanne nchini Uswizi, Ijumaa usiku.

Bingwa wa Jumuiya ya Madola Kinyamal aliongoza Wakenya wenzake Ferguson Rotich na Emmanuel Korir kufagia nafasi 1-2-3 katika mbio za mita 800. Wote watatu waliweka muda yao bora msimu huu baada ya kukamilisha mizunguko hiyo miwili kwa dakika 1:43.78, 1:43.93 na 1:44.01.

Korir atajilaumu mwenyewe kwa kuchukua uongozi kutoka kwa raia wa Puerto Rico Wesley Vazquez katika kona ya mwisho kabla ya kupunguza kasi yake na kupitwa na Kinyamal na Rotich. Vazquez aliishiwa na pumzi na kumaliza katika nafasi ya saba katika kitengo hiki kilichovutia wakimbiaji 11.

Watimkaji 16 walianza mbio za mita 1,500, lakini kasi ya juu ikafanya Wakenya Boaz Kiprugut, Ronald Kwemoi na Timothy Sein kusalimu amri kabla ya kukamilisha mizunguko yote mitatu.

Hata hivyo, mshindi wa medali ya fedha kwenye Riadha za Dunia, Jumuiya ya Madola na Bara Afrika Cheruiyot, ambaye amekuwa akitetemesha katika kitengo hiki mwaka huu, alidhihirisha uweledi wake kwa kutwaa taji kwa kasi ya juu mwaka huu ya dakika 3:28.7. Kasi hii ni rekodi mpya ya duru ya Lausanne. Alifuta rekodi ya dakika 3:29.51 ambayo raia wa Algeria Ali Saidi Sief aliweka mwaka 2001.

Bingwa wa Bara Ulaya Jakob Ingebrigtsen kutoka Norway aliyetimka mzunguko wa mwisho kwa kasi ya kutisha, aliridhika katika nafasi ya pili (3:30.16) naye raia wa Djibouti Ayanleh Souleiman akafunga tatu-bora (3:30.79).

Wakenya Vincent Kibet, Bethwell Birgen na Justus Soget walikamilisha katika nafasi za saba, 11 na 13, mtawalia.

Kenya iliona vimulimuli katika mbio za mita 5,000 pale mkimbiaji wake bora kukamilisha mizunguko hii 12 na nusu alikuwa Paul Tanui katika nafasi ya saba.

Ethiopia ilinyakua nafasi tatu za kwanza kupitia kwa Yomif Kejelcha, Selemon Barega na Telahun Bekele. Mganda Joshua Cheptegei, ambaye amekuwa akitifulia wenzake vumbi, alirushwa hadi nafasi ya nne.

Wanariadha 24 washiriki

Wakenya Nicholas Kimeli, Davis Kiplangat na Richard Yator walikamilisha katika nafasi za nane, tisa na 11 mtawalia, huku Cornelius Kangogo akishindwa kutamatisha. Wakiambiaji 24 walishiriki kitengo hiki.

Jepkosgei, ambaye alikuwa Mkenya wa pekee kati ya washiriki 10 kwenye mbio za mita 800 za wanawake, alikamilisha umbali huo kwa dakika 1:59.54.

Hii ni sekunde 0.43 mbele ya Mganda Halimah Nakaayi naye Gabriela Gajanova kutoka Slovakia akamaliza wa tatu (2:01.25).