Michezo

MASA yashinda Pre-Season Cup tayari kuanza ligi

July 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

MASA FC imehifadhi taji la KYSD Pre-season Cup kwa wasiozidi umri wa miaka 14 baada ya kuvuna bao 1-0 dhidi ya Kinyago United katika fainali iliyosakatiwa Uwanjani KYSD, Nairobi. Ngarambe hiyo huandaliwa kila mwaka wiki moja kabla ya mechi za Ligi ya KYSD kukunjua jamvi.

Licha ya Kinyago United ya kocha, Anthony Maina kuzua ushindani wa kusisimua ilijipata njiapanda baada ya Washington Onyango kutingia MASA bao la pekee dakika chache kabla ya kipenga cha mwisho.

”Kando na uhondo wa soka huandaa mechi za KYSD Pre-Season Cup kupima chipukizi wetu kabla ligi kuanza,” kocha huyo wa Kinyago United pia ofisa mkuu wa KYSD, alisema na kuongeza hatua hiyo huwapa wachezaji hao nafasi kutangamana.

Nao chipukizi wa Volcano FC waliibuka tatu bora baada ya kuranda Fernabache FC bao 1-0. Washington Onyango (MASA) na Peter Gathuri (Kinyago United) walitwaa tuzo ya mchezaji bora na golikipa bora. Kwenye nusu fainali Kinyago United iliichoma Volcano FC mabao 2-0 nayo MASA ilichuna magoli 5-1 mbele ya Fernabache FC

”Ingawa timu yangu ilibanduliwa kwenye mchujo mechi za KYSD Pre-Season zimeashira wazi kuwa ligi ya 2019/2020 itakuwa nomaree,” kocha wa Sharp Boys, Bonface Kyalo alisema na kujigamba kuwa ameandaa kikosi chake thabiti kuelekea uzinduzi wa ngarambe hiyo.

Nahodha wa MASA, Talena Ochieng akipokezwa kombe la Top 8 baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye mechi hizo ilipofungwa bao 1-0 na Kinyago United katika fainali. Picha/ John Kimwere

Kadhalika alisema Kinyago United, Sharp Boys na MASA zinapigiwa upatu kuteremsha upinzani wa kufa mtu kwenye mechi za kipute cha msimu huu.

Kocha wa Kinyago United, Anthony Maina naye alikiri kuwa ligi y msimu huu kamwe haitakuwa rahisi.

”Bila kuegemea upande mmoja vijana wanazidi kuimarisha mchezo wao hali inayoweka wazi kuwa wamejipanga kutifua kivumbi kikali kufukuzia ubingwa wa ligi msimu huu,” alisema na kuongeza kuwa la mno timu zote zimepania kujituma kiume ili kupokonya Kinyago United kombe la ligi hiyo.

Kinyago United imeshinda taji hilo mara 12 mfululizo. KYSD inajivunia kumlea Keithi Imbali ambaye huchezea Gor Mahia Youth inayotazamiwa kupandishwa ngazi kushiriki Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza msimu ujao.

Timu 16 zitashiriki kipute cha msimu mpya 2019/2020 ambazo ni:Kinyago United, MASA, Sharp Boys, Young Elephant, Locomotive, Blue Boys, Young Achievers, State Rangers, Black Jack, Gravo Legends, Lehmans, Volcano, Fearless, Spartans, Fernabache na Pumwani Ajax.