• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 6:55 AM
TZ yatimua kocha kwa kuondoka Afcon bila ushindi

TZ yatimua kocha kwa kuondoka Afcon bila ushindi

Na GEOFFREY ANENE

TANZANIA ni nchi ya hivi punde kuwa bila kocha baada ya Emmanuel Amunike kupigwa kalamu kwa sababu ya Taifa Stars kumaliza Kombe la Afrika (AFCON) linaloendelea nchini Misri, bila alama.

Likitangaza hatua ya kutengana na shujaa huyo wa zamani wa Nigeria, Shirikisho la Soka nchini Tanzania limesema Julai 7, “TFF na Kocha wa Timu ya Taifa “Taifa Stars” Emmanuel Amunike tumefikia makubaliano ya pamoja kusitisha mkataba baina yetu.”

Shirikisho hilo limeongeza, “TFF itatangaza Kocha wa muda atakaekiongoza Kikosi cha Timu ya Taifa kwa mechi za CHAN.”

Kabla ya Tanzania, Uganda ilitangaza kutengana na Mfaransa Sebastien Desabre baada ya kubanduliwa nje ya kipute cha AFCON kwa kulazwa na Senegal 1-0 katika raundi ya 16-bora Julai 5.

Wenyeji Misri walifuata mkondo huo kwa kupiga kalamu raia wa Mexico Javier Aguirre ya Afrika Kusini kuwalima 1-0 katika mchuano mwingine wa kuingia robo-fainali mnamo Julai 6.

Makocha zaidi huenda wakatimuliwa kutegemea umbali watakaofikisha timu zao kulingana matarajio ya mataifa wanayonoa na malengo waliyowekewa.

Indomitable Lions ya Cameroon, ambayo ilikuwa ikitetea taji, ilichapwa 3-2 na Nigeria katika raundi ya 16-bora na kuweka Mholanzi Clarence Seedorf pabaya kutemwa. Morocco pia huenda ikaamua kutema kocha Mfaransa Herve Renard, ambaye timu yake ya Atlas Lions ilizimwa na Benin kupitia penalti 4-1 baada ya muda wa kawaida na ule wa ziada kumalizika 1-1.

Tanzania ilipoteza 2-0 dhidi ya Algeria, 3-2 dhidi ya Kenya na 3-0 dhidi ya Senegal katika mechi za Kundi C jijini Cairo. Mashabiki wa Kenya nao wamegawanyika kuhusu kuendelea kwa Mfaransa Sebastien Migne kuwa kocha mkuu ama atimuliwe baada ya Harambee Stars kubanduliwa nje katika mechi za makundi baada ya kulemewa 2-0 na Algeria na 3-0 dhidi ya Senegal na kushinda Tanzania 3-2.

Migne alielekea nchini mwake Ufaransa baada ya mechi ya mwisho ya Kenya, huku Shirikisho la Soka nchini (FKF) likisema amechua likizo ya wiki moja.

Kenya na Tanzania zitakutana katika mechi ya kufuzu kushiriki soka ya wachezaji wanaosakata katika mataifa yao almaarufu CHAN baadaye mwezi huu wa Julai.

You can share this post!

Vishale: Nairobi Stima na Trans Nzoia zaanza vyema

Uamuzi wa kesi ya uchochezi dhidi ya Kuria waahirishwa

adminleo