MAPOZI: Nviiri
Na PAULINE ONGAJI
HUENDA baadhi wamemfahamu baada yake kushirikishwa kwenye kibao Extravaganza na Sauti Sol.
Ukweli ni kwamba Nviiri the Storyteller kama anavyofahamika miongoni mwa mashabiki wake, amekuwepo ulingoni kwa muda.
Ustadi wake unadhihirika kwani ni mmojawapo wa wanamuziki waliochaguliwa kupamba tamasha ya muziki ya Hype Festival 2019 jijini Nairobi na hivyo kuungana na majina makubwa kama vile mwanamuziki kutoka Nigeria, Maleek Berry.
Kwa wanaoshuku ushupavu wake kama mtunzi, ni muhimu kuwajulisha kwamba alishirikiana na Sauti Sol katika uandishi wa kibao Melanin, kilichowapa umaarufu nchini Kenya na mbali, huku kikiendelea kuvutia watazamaji zaidi ya milioni 15 kwenye mtandao wa YouTube.
Ni ustadi huu uliomfanya Nviiri ambaye pia ni mcheza gita na mhariri wa video, kuwa mmojawapo wa wasanii wachache ambao wamesajiliwa chini ya lebo ya Sol Generation Records, yao Sauti Sol.
Mbali kidogo na muunganisho wake na bendi hii, Nviiri pia amejiundia jina kupitia nyimbo zake ambapo anafahamika kwa vibao kadha; kimojawapo kikiwa ni wimbo Pombe Sigara ambao kinyume na kichwa chake, unazungumzia mapenzi kwa mabinti.
Aidha anafahamika kwa vibao vingine kama vile Penzi, suala ambalo linathibitisha mvuto wa ujumbe wa mahaba kwa kila kazi anazoshughulikia.
Kama mwandishi wa nyimbo, pia amepata fursa ya kushughulikia kazi za baadhi ya wanamuziki wa injili na nyimbo za kilimwengu.
Na ni uwezo huu wa kutobagua wasanii anaowafanyia kazi ambao umemtenga na wengine wanoshughulika katika fani ya uandishi wa nyimbo.
Siri yake ni gani?
Aidha, siri yake imekuwa kufanya kolabo na wasanii maarufu ili kufikia kiwango chao.
Pia, uwezo wa kuhaisha kazi zake, umemwezesha kupata shavu zaidi.
Hii haimaanishi kwamba hajakumbana na changamoto katika harakati hizi.
Kwa mfano. alipoanza kuandika nyimbo, haikuwa rahisi kwake kwani soko la muziki la hapa nyumbani lilimpa chenga kiasi.
Hata hivyo alipata ujasiri na nguvu kwa kushirikishwa katika uandishi wa kibao Melanin.
Ili kukabiliana na changamoto ya kunakiliwa kwa ngoma zake, amekuwa akisajili kila kazi anayoifanya.
Mbali na hayo, siri yake pia imekuwa kusikiza kazi za wanamuziki mbalimbali, vile vile kuwa na ufahamu wa mambo mengi yanayohusiana na burudani.
Fursa yake ya kuandikia kibao mojawapo ya bendi maarufu barani lilimjia baada ya kuwafanyia kazi kama produsa wa video. Ni hapa mkoko ulialika maua.
Licha ya kwamba hajakita mizizi katika tasnia ya muziki, umaarufu wake umekuwa ukiongezeka. Ni hali inayotarajiwa kuendelea hasa ikizingatiwa kwamba amebahatika kuwa mmoja wa wasanii wachache waliofichwa chini ya ubawa wa Sauti Sol, na ni bidii yake tu itaamua iwapo atadumu au kuchujuka.