SHANGAZI AKUJIBU: Nimepata demu tajiri aliyenizidi umri anayedai kunipenda
Na SHANGAZI
SHANGAZI natumai wewe ni mzima. Tafadhali nahitaji ushauri wako. Nina umri wa miaka 20 na kuna mwanamke mwenye umri wa miaka 25 anayeniambia ananipenda. Ana mtoto mmoja na ni tajiri sana licha ya umri wake mdogo. Waonaje?
Kupitia SMS
Iwapo nimekuelewa vizuri, mwanamke huyo ndiye anayekupenda, wewe huna haja naye. Kama hali ni hiyo, usikubali kuingia katika mtego wake eti kwa sababu ni tajiri ilhali humpendi. Mapenzi ya pesa kamwe hayadumu. Ninaelewa kuwa ni vigumu kumkatalia mwanamke ombi lake. Lakini kumbuka kuwa mwanamke huyo anakutaka uwe mwenzake maishani kwa hivyo itakuwa makosa kumkubali ukijua kwa hakika kwamba huna hisia kwake. Mwambie ukweli ingawa mchungu.
Tulipanga kuoana sasa ananipuuza
Habari zako shangazi? Nimekuwa na mchumba na tulikuwa tumekubaliana kufunga ndoa hivi karibuni. Hata hivyo tumekosana kuhusu jambo fulani na sasa hataki kuongea nami. Nimempigia simu na kumtumia SMS mara nyingi nikitaka tushauriane na kusuluhisha jambo hilo lakini amepuuza. Nifanye nini?
Kupitia SMS
Kukosana ni jambo la kawaida miongoni mwa binadamu, iwe ni kati ya wapenzi, jamaa au marafiki. Ingawa hujaelezea ni jambo gani lililowafanya mkosane, mchumba wako hana sababu nzuri ya kukatiza mawasiliano hasa baada yako kujitolea kumtafuta ukitaka suluhu. Kwa upande wako, umetimiza wajibu wako katika juhudi za kudumisha uhusiano wenu. Sasa mpe muda hata kama ni miezi kadhaa. Asipokutafute basi ujue ameamua huo ndio mwisho wa uhusiano wenu.
Nahisi penzi letu limekuwa baridi sijui utanisaidia vipi
Shangazi pokea salamu zangu. Nina umri wa miaka 22 na kuna mwanamume ambaye tumependana kwa miaka miwili sasa. Sielewi ni kitu gani kinaendelea kwani ghafla amekuwa baridi hata kunipigia simu ni shida ilhali awali alikuwa akinipigia mara kadhaa kwa siku. Inawezekana amepata mwingine?
Kupitia SMS
Hizo si dalili nzuri katika uhusiano. Hatua ya mwenzako ya kukatiza ghafla mawasiliano inaweza kuwa ujumbe kwako kwamba ameamua kujiondoa katika uhusiano huo na hataki ama anaogopa kukwambia wazi. Ikiwezekana mtafute umuulize ili ujue ukweli kutoka kwake mwenyewe.
Amekwamilia tunda, asema hadi amalize masomo yake
Vipi shangazi. Nina uhusiano na mrembo fulani mwanafunzi wa shule ya upili. Hata hivyo, amekataa kabisa na tunda lake akisema ni lazima kwanza amalize masomo. Nampenda sana kwa hivyo nimekubali kauli yake na nimeamua kusubiri. Je, anaweza kunigeuka wakati huo ukiwadia?
Kupitia SMS
Iwapo huna habari, ni haramu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mtoto wa shule na haramu hata zaidi kudai tendo la ndoa kutoka kwake. Ninaamini kuwa yeye mwenyewe anajua hivyo na ndiyo maana amekataa ombi lako. Hata asipotimiza ahadi yake baada ya masomo, hiyo si haki yako na hutakuwa na budi ila kuheshimu kauli yake.
Mimi ni mwanafunzi na mpenzi ataka eti nimzalie kwanza
Shikamoo shangazi! Kuna kijana ambaye tumekuwa wapenzi kwa miaka minne sasa. Anasema anataka nimzalie mtoto lakini siko tayari kwa sababu mimi bado ni mwanafunzi wa shule ya upili. Sasa anatishia kuniacha. Nifanye nini?
Kupitia SMS
Masomo na mapenzi ni mambo mawili ambayo hayawezi kuchanganywa na wanaojaribu huambulia patupu. Wazazi wako wanajitolea kukusomesha ili uweze kujikimu kimaisha baadaye na ni makosa makubwa kwako kuingilia mapenzi kwani yataathiri vibaya masomo yako. Isitoshe, eti unataka ushauri wangu kuhusu iwapo unafaa kumzalia mpenzi wako ili aije akakuacha? Shauri yako.