• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 8:55 AM
Teknolojia ya VAR ingetufaa pakubwa, asema kocha wa Ghana

Teknolojia ya VAR ingetufaa pakubwa, asema kocha wa Ghana

Na MASHIRIKA na CECIL ODONGO

KOCHA wa timu ya taifa ya Ghana Kwesi Appiah amesikitika vijana wake kubanduliwa kutoka kipute cha Mataifa Bingwa Barani Afrika (AFCON) kinachoendelea nchini Misri akisema mambo yangewaendea vyema ikiwa teknolojia ya VAR ingetumika.

Black Stars ya Ghana ilitupwa nje na Tunisia 5-4 kupitia mikwaju ya penalti baada ya timu hizo kutoka sare ya 1-1 katika muda wa kawaida na dakika 30 za muda wa ziada.

Bao walilofunga kipindi cha kwanza kupitia Andrew Ayew lilikataliwa, wasimamizi wa mechi wakisema kiungo Thomas Partey aliunawa mpira huo kabla ya kumfikia Ayew.

“Tulikuwa na nafasi kadhaa kufunga mabao katika vipindi vyote viwili. Iwapo teknolojia ya VAR ingetumika kuamua uhalali wa bao letu, matokeo yangekuwa vinginevyo,” akasema Appiah baada ya mchuano huo kukamilika.

Mkufunzi huyo ambaye zamani alikuwa nahodha wa Black Stars pia alikiri kwamba walitamalaki mchezo wote lakini wakakosa kuadhibu Tunisia mapema kabla ya mechi kukamilika.

“Katika mechi ya soka, unaweza kubuni nafasi kadhaa za kufunga lakini ukikosa bahati basi kivyovyote huwezi kushinda. Kwa kuwa VAR inatumika duniani na tunajua umuhimu wake, Shirikisho la Soka Afrika linafaa kuitumia teknolojia hiyo ili kupunguza makosa yanayotendwa kila mara na waamuzi wa mechi,” akaongeza.

Kabla ya mchuano huo kuanza, CAF ilitoa tangazo kwamba teknolojia ya VAR ingetumika kuanzia awamu ya robo fainali jambo ambalo Appiah hakubaliani nalo akisema makosa ya maamuzi kwenye mechi ya makundi na mwondoano yangeepukika iwapo VAR ingetumika mechi zote.

“Katika makala yajayo ya CAF, VAR inafaa kutumika katika mechi zote ili kuipa Afcon hadhi kama michuano ya mabara mengine. Sipendi kushtumu maamuzi ya marefa lakini natumai ataangalia video ya bao alilokataa na kujihukumu au kujiondolea lawama,” akasisitiza.

Tunisia inatarajiwa kukutana na Madagascar kwenye robo fainali Alhamisi Julai 11.

You can share this post!

Pogba, Lingard waonekana wakizozana

Maafisa waadilifu wa trafiki kutuzwa

adminleo