Makala

KINA CHA FIKIRA: Unominishaji bandia wa neno 'lalama' unakirihi

July 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na KEN WALIBORA

KATIKA makala hii tunajadili baadhi ya makosa yaliyoshamiri katika matumizi (zingatia kwamba nimetumia kauli “makala hii,” suala ambalo nitalirejelea baadaye).

Kwanza kuna matumizi ya neno “lalama” yanayolifanya liwe nomino. Utawasikia watu, hasa wanahabari wakisema, “lalama hizo” au “lalama zao.” Neno lalama halifai kulazimishwa kuwa nomino.

Huu unominishaji bandia ni kuharibu lugha makusudi.

Tutazama mifano kadha ya fasili ya neno hili ambalo sikuzote linawekwa katika kategoria ya kitenzi wala si nomino:

Kamusi Teule ya Kiswahili: “1. taka msamaha, 2 lia kwa kelele.”

Kamusi ya Kiswahili-Kiingereza, TUKI: “complain, carp, yammer “

Kamusi ya Karne ya 21: “toa sauti au lia kwa kelele .”

Kamusi ya Kiswahili Fasaha: “1 kitendo cha kutoa maelezo yenye hisia ya kutoridhishwa na jambo. 2 kitendo cha kutoa sauti ya kuumia.

Kamusi Kuu ya Kiswahili a. toa sauti kubwa agh. kelele yenye kuhitaji msaada wa dharura. b sema maneno yenye hoja kuntu za kujitetea au kuhitaji jambo fulani lifanyike ch. omba radhi ama msaada agh. kwa Mungu; fanya toba.”

Je, pana popote katika katika kamusi hizi zote ambapo dhana ya “lalama hizo” au “lalama zako” imedokezwa, yaani matumizi ya neno “lalama” nje ya kategoria ya kitenzi? Hakuna.

Kwa hiyo watu wa kawaida, lakini hasa wanahabari (hata wa Nation Media Group), waache kutuzuzua kwa kutumia kitenzi “lalama” kinomino, badala ya kutumia nomino mwafaka katika muktadha kama vile “malalamishi” au “malalamiko.”

Makala

Pale juu nimetumia kauli “makala hii.” Kama zingekuwa nyingi ningesema au kuandika “makala hizi.”

Huu ni uteuzi wa maneno sahili, sahihi, na yasiyokuwa na utata.

Simaanishi kwamba mtu asemapo “makala haya” anakosea. “Makala haya” pia ni sahihi, lakini haina usahili hasa unapojaribu kutofautisha kati ya hali ya umoja na wingi.

Kwa hivyo ,“makala haya” ni kauli sahihi lakini ambayo inaleta utata wa kupambanua umoja na wingi, utata ambao haumo katika kutumia “makala hii/ makala hizi.”

Ninachosema ni kwamba katika umoja tutasema “makala haya” na katika wingi tutasema pia “makala haya,” na kuzua usahihi ambao umesheheni utata au mkanganyiko.

Ndiyo maana napendekeza kwa dhati ya moyo matumizi ya makala hii/hizi. Wale wanaojificha katika kwapa za usahihi wakisema “makala hii/makala hizi” si sawa au kutumia “lalama” kuwa nomino, wanajidanganya wenyewe.