Mishahara: Lusaka atetea wabunge na maseneta
Na CHARLES WASONGA
SPIKA wa Seneti, Ken Lusaka ametetea mtindo wa wabunge na maseneta kutaka waongezewe mishahara na marupurupu akisema hali huchangiwa na mzigo walio nao wa kuridhisha mahitaji ya wananchi.
Akihojiwa Alhamisi asubuhi katika Radio Citizen Bw Lusaka amesema malipo ya wabunge na maseneta sio ya juu zaidi inavyodai yalinganishwa na yale ambayo maafisa wengine wakuu wa serikalini na katika Idara ya Mahakama hupokea kila mwezi.
“Japo kikatiba wabunge na maseneta pia huchukuliwa kuwa maafisa wa serikali, itapata kuwa wao kusukumwa na wananchi wakitaka misaada mbalimbali kama vile pesa za harambee, za kugharamia mazishi, bili za hospitali na mahitaji mengineyo. Bila shaka hii ndio maana wanaitisha mishahara na marupurupu zaidi,” akasema Lusaka.
“Kila asubuhi, Mbunge au Seneta anapaoamka kwake hukumbana na zaidi ya watu 50 wakitaka misaada mbalimbali kutoka kwake. Hali kama hii huwa haishuhudiwa katika makazi ya majaji, mawaziri au makatibu wa wizara,” Bw Lusaka akaongeza.
Alikuwa akitoa kauli yake kuhusu habari kwamba wabunge wametuma mapendekezo kwa Tume ya Kukadiria Mishahara ya Watumishi wa Umma (SRC) wakitaka malipo yao yaongezwe.
Wanapendekeza walipwe marupurupu kadhaa yakiwemo yale ya malazi wanapohudhuria vikao vya bunge jijini Nairobi ya kima cha Sh24,000 kila wiki.
Pamoja na nyongeza ya marupurupu mengine, kwa ujumla wabunge wanataka wawe wakipokea Sh2.9 milioni kila mwezi kutoka Sh1.1 milioni wanazopokea sasa.
Bw Lusaka aliwataka wananchi kukoma kuwachukulia wabunge na maseneta kama suluhu kwa matatizo yao yote “kwani hiyo ndio sababu inayofanya viongozi hao kuitisha malipo ya juu.”
Ubabe
Kuhusu vita vya ubabe kati ya Seneti na Bunge la Kitaifa, Spika Lusaka alisema havifai kuwepo kwa sababu katiba imebainisha wazi majukumu ya mabunge hayo.
“Sioni haja ya kuwepo kwa mivutano hapa kwani kipengee cha 96 cha Katiba kinasema wazi kuwa Seneti inapaswa kushughulika na masuala yote ya kaunti. Na kipengele cha 95 kinasema masuala yanayohusu serikali ya kitaifa yanapasa kushughulikiwa na bunge la kitaifa,” akasema.
Wiki jana maseneta walisema watakwenda mahakamani kutaka kubatilishwa kwa miswada 23 ambayo ilipitishwa na wabunge bila mchango wao ilhali yanahusu kaunti.
Na wabunge pia wamelalama kuwa maseneta huingilia kazi za kwa kuwaita mawaziri ambao wizara zao hazihusiani na majukumu ya kaunti.
Hii ndio maana wiki jana kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa Aden Duale aliwashauri mawaziri Fred Matiang’i (Usalama wa Ndani), Rachel Omamo (Ulinzi) na Monica Juma (Masuala ya Kigeni) kukaidi miali kutoka kwa kamati za seneti.