Kenya kuunda kikosi cha Cecafa U-17
Na GEOFFREY ANENE
TAREHE za mashindano ya soka ya kimataifa ya wavulana wasiozidi umri wa miaka 17 ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa Under-17 Challenge Cup) zimetangazwa. Kenya iko katika harakati ya kuunda kikosi.
Kulingana na Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), Burundi itakuwa mwenyeji wa mashindano haya kutoka Aprili 1 hadi Aprili 15, 2018.
Burundi ilifaa kuandaa kombe hili jijini Bujumbura mnamo Desemba mwaka 2017, lakini likaahirishwa.
Mara ya mwisho mashindano haya yalifanyika ni mwaka 2009.
Uganda, ambayo iliandaa makala hayo, iliibuka mshindi kwa kulima Eritrea 2-0 katika fainali. Kenya ilitolewa mapema katika mechi za makundi ilipobwagwa 1-0 na Ethiopia, ikapepetwa 4-1 na Uganda na kupoteza 3-1 dhidi ya Zanzibar.
Makala ya kwanza yaliandaliwa mwaka 2007 nchini Burundi ambapo Kenya ilizoa medali ya shaba baada ya kulemea Rwanda kwa njia ya penalti 5-3 baada ya muda wa kawaida kumalizika 2-2. Burundi ilicharaza Uganda 2-0 katika fainali.
Wanachama wa Cecafa ni Kenya, Rwanda, Burundi, Uganda, Tanzania, Zanzibar, Ethiopia, Sudan, Sudan Kusini, Djibouti, Somalia na Eritrea.