Makala

KILIMO: Mimea inyunyiziwe maji kwa wingi baada ya kupuliziwa dawa

July 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na SAMMY WAWERU

WATU wengi nchini hutumia mboga na viungo mbalimbali vya mapishi kila siku.

Mboga inayoongoza katika orodha ya zinazoliwa mno ni sukumawiki, ikifuatwa na spinachi na kabichi.

Vilevile, kuna wanaothamini mboga za kienyeji au zile asili kama mnavu, mchicha, kunde, kansella, saga, miongoni mwa nyinginezo.

Viungo kama nyanya, vitunguu, pilipili mboga, mamumunya na giligilani maarufu kama dania, hutumika mara kwa mara katika mapishi. Aidha, viungo hivyo vinaaminika kuongeza ladha kwenye chakula.

Mboga na viungo huzalishwa shambani, na kabla kuvunwa huwa vimepitia hatua mbalimbali.

Kuna wakulima wanaozingatia mfumo wa kilimohai, upanzi kwa kutumia mbolea hai – mifugo na mboji – ambapo huzalisha mazao bila kutumia kemikali yoyote.

Hii ina maana kuwa hawatumii fatalaiza yoyote ile wala kupulizia dawa dhidi ya wadudu na magonjwa, kwani wanakumbatia kilimo asilia.

Katika hali hiyohiyo, wakulima wengine hupanda kwa fatalaiza ya kisasa ikiwa ni pamoja na kupulizia dawa kukabili changamoto za magonjwa na wadudu. Pia, hutumia mbolea ya kisasa kunawirisha mazao.

Kwa sababu ya matumizi ya kemikali katika upanzi na utunzaji wa mimea, mkulima anashauriwa kuinyunyizia maji kwa wingi hususan baada ya kuipulizia dawa.

Kulingana na wataalamu wa masuala ya afya wanasema hili litasaidia pakubwa katika jitihada za kukabiliana na magonjwa ibuka yanayohusishwa lishe.

“Baadhi ya maradhi yanatokana na uchafu wa lishe tunayokula, kemikali ikiwa mojawapo ya kichangio kikuu,” anasema Mary Ann Njeri, mtaalamu kutoka Hospitali ya Ladnan jijini Nairobi.

Anasema changamoto za aina hiyo zitadhibitiwa endapo wakulima wataitikia kunyunyizia mimea maji kwa wingi baada ya kuipulizia dawa dhidi ya wadudu na magonjwa.

“Mazao yanapaswa kuvunwa siku 14 baada ya kuyapulizia dawa. Muda huo wewe kama mkulima utumie kunyunyizia mimea maji kwa wingi,” ahimiza Bi Njeri, hatua inayoungwa mkono na Bw Simon Wagura, mtaalamu wa kilimo na mwanzilishi wa The Country Farm, shirika linaloangazia upanzi, utunzaji na uzalishaji wa mimea na wanyama lenye makao yake eneo la Ruiru.

Bw Simon Wagura, mtaalamu wa masuala ya kilimo na mwanzilishi wa The Country Farm, shirika linaloangazia ukuzaji wa mimea na utunzaji wa wanyama, akinyunyizia mboga maji. Picha/ Sammy Waweru

“Ni hatari kupulizia mazao dawa ya kuua wadudu na kudhibiti magonjwa kisha kuvuna mara moja na kupeleka sokoni bila kuyanyunyizia maji kwa wingi. Siku 14 ni muhimu kuwezesha dawa kuisha kwenye mazao,” anasema Bw Wagura ambaye pia ni mkulima wa mboga Ruiru.

Kukiwa na jua kali, athari za wadudu hushuhudiwa mara kwa mara. Hali kadhalika, magonjwa yanayohusishwa na baridi hujitokeza msimu wa mvua.

Ili kukwepa hasara za wadudu na magonjwa, wakulima hupulizia mazao dawa zingine zikikisiwa kuwa na kemikali.

“Kilimo cha mahema kinasaidiwa kuangazia suala la wadudu na magonjwa yanayosambazwa na upepo,” anaeleza Bw Mwae Malibet, mkulima wa mboga kwenye hema (green house) Gachie, Kiambu.

Hukuza mboga aina ya spinachi na sukumawiki.

Hata hivyo, anasema magonjwa ya mboga hayakosi kujiri hata kwenye hema.

Bw Brian Mbugua, mkulima wa pilipili mboga na nyanya kwenye hema Tigoni, eneo la Limuru, Kiambu anapendekeza haja ya kampuni za dawa kuunda zisizo na kemikali.

Kulingana naye gharama ya upanzi na utunzaji wa mazao huwa ghali na ndiposa sharti adhibiti changamoto zinazoibuka.

“Haja ipo kampuni za kuunda fatalaiza na dawa zizingatie usalama wake. Ikumbukwe kuwa sisi wakulima ndisi walaji wa kwanza wa mazao yetu. Pia, ni muhimu tutilie maanani unyunyiziaji wa maji kwa wingi kwa mimea tunapoipulizia dawa,” aelezea Bw Mbugua, kauli yake ikitiliwa mkazo na Malibet.

Wakulima hawa pia wanahimiza serikali kuweka sheria kali zitakazotathmini uundaji wa fatalaiza na dawa.

“Mteja anaponunua mazao ya kilimo ahakikishe ameyaosha sawasawa kwa maji ili kuyasafisha,” wanashauri.

Bi Mary Anne Njeri, mtaalamu wa afya, anatilia mkazo umuhimu kuosha matunda kabla ya kula.

“Kuna baadhi ya watu wanaokula ndizi au machungwa sokoni bila kuyaosha eti kwa sababu yana maganda wanayoyaotoa. Ni hatia, vidole unavyotumia kuyaondoa ndivyo utavitumia kushika matunda, yaoshe kabla kuyachambua,” asisitiza.

Isitoshe, mdau huyu anaeleza haja ya kuosha viungo vya mapishi kabla ya kuvitumia. Anasema kwa kufanya hivyo magonjwa kama Saratani-ndwele ambayo imekuwa sugu, yatadhibitiwa.