Makala

SIHA NA LISHE: Manufaa ya kula kabichi

July 12th, 2019 1 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

KABICHI linaweza kuliwa bichi, likachanganywa kwenye kachumbari au kupikwa na kula. Kabichi lina vitamini C, madini ya calcium na chuma.

Linaponyesha vidonda vya tumbo linapotumika katika mfumo wa juisi. Ukishamaliza kutengeneza juisi, ni vyema kuinywa mara moja kabla haijakaa sana.

Glasi moja ya juisi ya kabichi inasaidia kuondoa mhemko au msongo kwenye akili na pia kama kichwa kinawanga.

Kwa tatizo la pumu, chukua juisi ya karoti ongeza na juisi ya spinachi na uinywe.

Pia unaweza kula kachumbari ya kabeji na spinachi bila chakula kingine muda wowote.

Kwa kachumbari, changanya nyanya, kitunguu maji na limau kidogo na kabichi.

Vidonda vya tumbo

Juisi ya kabichi inaelezwa kuwa na faida nyingi tumboni, hasa kwa wale wenye matatizo ya vidonda vya tumbo (peptic ulcers). Ikitumika mara kwa mara huwa kama tiba kwao. Hali kadhalika husaidia kwa mfumo wa usagaji chakula tumboni.

Mfumo wa moyo

Mboga hii huimarisha mfumo mzima wa moyo kwa kudhibiti utengenezwaji wa lehemu (cholesterol) mbaya mwilini ambayo inapozidi mwilini, husababisha matatizo ya moyo.

Vitamini

Ndani ya kabichi, kuna kiwango cha kutosha cha aina mbalimbali za vitamini, kama Vitamini K, Vitamini B1, Vitamini B2, Vitamini A na Vitamini C.

Kabichi ina kiasi kingi cha kambalishe (fiber), Manganizi (Manganese), Potasiamu (Potassium) na Fatty-3 acids.

Vyote hivi ni kinga ya mwili dhidi ya magonjwa nyemelezi.