• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
‘Dozi’ ya mama pima yaleta balaa

‘Dozi’ ya mama pima yaleta balaa

Na NICHOLAS CHERUIYOT

KONOIN, BOMET

KULITOKEA kioja eneo hili jamaa alipomtimua mama pima kwa kujaribu kumpelekea baba yake anayeugua dozi kisiri.

Kwa mujibu wa mdokezi, baba ya jombi ni mraibu sugu wa dozi na juzi alipougua, jamaa aliomba ruhusa anakofanyia kazi ili kumshughulikia hadi apate nafuu.

“Baadhi ya masharti aliyopewa mgonjwa huyo ni kuwa lazima aweke breki unywaji wa pombe hadi afya yake iimarike. Jombi alimshauri baba azingatie maneno ya daktari na kuapa kuhakikisha mzee hangekaribia kopo la dozi,” mdaku alieleza.

Juzi, jamaa alirudi kutoka matembezini na kupata mzee amepiga mtindi. Alipomuuliza ni nani aliyempa pombe hiyo, mzee alinguruma kwamba alikuwa amepata nafuu kiasi cha kuanza kukata kiu polepole.

“Usinirushie maswali kijana, ninahisi buheri wa afya. Naamini daktari alitia chumvi ubaya wa pombe kwa afya yangu,” mzee alinguruma naye kijana akafyata ulimi na kuamua kutumia mbinu nyingine kuzima pombe hiyo.

Siku iliyofuata, jamaa alijificha kichakani kumsubiri aliyekuwa akimpelekea baba yake pombe ili amtie adabu. Mara mzee alimpigia simu mama pima kumletea dozi haraka.

“Kimbia uniletee chupa ya kinywaji. Kijana ameenda kutangatanga mtaani,” mzee alisikika akipitisha ujumbe wa dharura kupitia simu.

Baada ya muda mfupi, jombi alimuona mama akitembea kwa kasi akihema, dozi mkononi. Jamaa alichomoka kichakani na kumkabili mama huyo.

“Ninajikaza kumtibu mzee lakini wewe unazidi kuharibu mambo kwa tamaa ya pesa,” jombi alimfokea mama pima. Kilichofuata kikawa ni sinema mama pima alipoamua mguu niponye naye akamkimbiza mbio.

You can share this post!

Baraza la kijeshi Sudan ladai lilitibua njama ya mapinduzi

NGUGI: Ukweli ni kwamba Wakenya walia; mzigo haubebeki

adminleo