Makala

NGUGI: Ukweli ni kwamba Wakenya walia; mzigo haubebeki

July 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MWITHIGA WA NGUGI

ULAFI wa viongozi wa kisiasa nchini umefikia viwango vya kutamausha.

Ukweli ni kwamba, wanasiasa wanawarubuni Wakenya, viti vyao vina joto ya pesa na ubwana, hivi kwamba wanaona walifika mwisho wa siasa.

Wakenya wanalia, kuanzia serikali za kaunti ushuru umekuwa mwingi kupita kiasi, na ndiposa tunasema punda amechoka ya kutosha. Kwa sasa tunafaa tuwe na katiba mpya, utawala mpya na serikali mpya.

Sisi wana mashinani tunalia kila siku kwa sababu ya askari na machifu wanao tuvunjia heshima zetu kwa boma kwa sababu ya kutumia nguvu kupita kiasi.

Tusiwe watu wa kulia kila siku; lazima tuchukue hatua sasa, wezi waheshimiwa hawafai kulindwa kila uchao; tumechoka. Ni miaka mingi tumezidi kulia na hasa ni kwa sababu ya wanasiasa watundu.

Huu si wakati wa kuwabembeleza wezi wa miwa (waheshimiwa) Kenya inahitaji waheshimiwa wa kuitumikia.

Wakenya wamechoka, tumekuwa na mzigo mkubwa wa kuwalipa viongozi waheshimiwa na ni wengi kupita kiasi. Kinachosikitisha zaidi ni kuona jinsi kama taifa, tumekuwa ombaomba wa kimataifa, serikali inakopa hapa, pale na huko.

Swali ni, tutakopa hadi lini? Badala ya kupunguza matumizi ya serikali, kinachohuzunisha ni kuona nyadhifa mpya zisizokuwepo kwenye katiba zikibuniwa za kuwazawadi ‘marafiki wa kisiasa’ nyadhifa ambazo tayari ni mzigo tosha kwa walipa ushuru.

Nani mwenye mamlaka?

Kenya tusijidanganye.

Katiba yetu i wazi kuhusu ni nani ana mamlaka.

Mkenya ndiye mwenye mamlaka yote na kwa hivyo hamna haja ya mwanasisa yeyote kujaribu au hata kuwatisha wananchi kuhusu nguvu zisizokuwepo za rais, kwa kifupi soma ibara ya kwanza ya Katiba yetu.

Uhuru wa Wakenya unafaa kuheshimiwa na viongozi wetu, ushuru wetu kamwe haufai kumezwa kama njugu karanga na watu wachache tukiangalia.

Tuna raslimali na fedha zinazoweza kumfaidi kila Mkenya lakini bora tu usimamizi wake uweze kusimamiwa kwa njia yenye uwazi na uwajibikaji. Ugatuzi wetu wa kikatiba kila uchao unatusababishia matatizo si haba.

Badala ya ugatuzi kugatua maendeleo na raslimali kwa wananchi mashinani kinachothibitika ni ufujaji wa fedha mashinani na kumfukarisha ‘Wanjiku’ hata zaidi.

Nikiwatizama wanasiasa, wakubwa kwa wadogo kwa uketo, wanachokipenda zaidi ni kuendeleza na kuhubiri maji ilhali wao ni ‘walevi’ wa mvinyo wa siasa za 2022 ambao kwa sasa wameufanya ibada yao na kuwasahau wananchi waliowatwika mataji ya uongozi.

Ada ya mja kunena muungwana ni vitendo, hebu niseme leo nazo nyayo zangu na zinifuate.