• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Harambee Starlets kuingia mazoezini Jumapili maandalizi mechi za kufuzu Olimpiki

Harambee Starlets kuingia mazoezini Jumapili maandalizi mechi za kufuzu Olimpiki

Na GEOFFREY ANENE

KIKOSI cha timu ya taifa ya soka ya wanawake ya Kenya almaarufu Harambee Starlets kitaingia kambini Jumapili kuanza kujiweka tayari kwa mechi za kufuzu kushiriki michezo ya Olimpiki mwaka 2020 nchini Japan.

Kenya haijawahi kushiriki soka katika Olimpiki katika historia yake. Itavaana na She-Flames ya Malawi mnamo Agosti 26 nchini Malawi na kualika timu hiyo nchini Kenya mnamo Septemba 1. Kuna raundi nne kabla ya Starlets kufika Japan.

Kocha David Ouma alitaja kikosi cha wachezaji 39 kwa majukumu hayo ya kutafuta tiketi ya Olimpiki.

Wachezaji wengi katika timu ya Kenya walishiriki mechi za kufuzu za Kombe la Afrika (AWCON) 2018 dhidi ya Uganda na Equatorial Guinea.

Starlets itakuwa na mazoezi ya siku tano, huku vipindi vya mazoezi zikifanyika katika uwanja wa Camp Toyoyo.

Kambi hii ya mazoezi itakatizwa Julai 19 kuruhusu wachezaji kujiunga na klabu zao kwa mechi za Ligi Kuu.

Kenya ilipata tiketi ya bwerere kuingia raundi ya pili baada ya kukosa mpinzani.

Timu ya taifa ya Malawi, ambayo ilianza maandalizi yake Julai 10, ilianza kampeni yake ya kufuzu katika raundi ya kwanza mwezi Aprili.

Malawi itatumia Kombe la Afrika ya Kusini (COSAFA), ambalo litaandaliwa Julai 31 hadi Agosti 11 mjini Port Elizabeth nchini Afrika Kusini, kujiweka tayari kwa mechi dhidi ya Kenya.

Vyombo vya habari nchini Malawi vimenukuu kocha Abel Mkandawire akisema ameridhishwa na timu yake baada ya siku ya kwanza ya mazoezi.

“Nimeridhishwa na wachezaji. Walichunguzwa kuiafya asubuhi (Julai 10) na wote wakawa katika hali nzuri.

“Tulikuwa na kipindi cha kwanza cha mazoezi (Julai 10 alasiri) na ilikuwa rahisi kuona bado hawajapoteza hali yao tangu kambi yetu ya mwisho mwezi Mei,” alisema.

She-Flames imekutanishwa na mabingwa watetezi Afrika Kusini pamoja na Madagascar na Comoros katika Kundi A kwenye COSAFA.

Malawi ilijikatia tiketi ya kukutana na Kenya katika raundi ya pili baada ya kuaibisha Msumbiji 11-1 Aprili 4, 2019 jijini Blantyre na kuilemea 3-0 katika mechi ya marudiano siku tano baadaye jijini Maputo.

Mshindi kati ya Kenya na Malawi atakabiliana na mshindi kati ya Gabon na Ghana katika raundi ya tatu mwezi Septemba/Oktoba na kisha mshindi kati ya Zambia/Zimbabwe na Botswana/Afrika Kusini katika raundi ya nne mwezi Novemba. Mshindi wa raundi ya tano atajikatia tiketi ya kushiriki Olimpiki nchini Japan mwaka 2020, huku nambari mbili akipata fursa ya mwisho ya kufika jijini Tokyo kwa kumenyana na Chile iliyomaliza soka ya Copa America katika nafasi ya pili nyuma ya Brazil mwezi Aprili mwaka 2018.

Kikosi cha Kenya

Makipa – Wilfrida Seda (Vihiga Queens), Judith Osimbo (Gaspo Youth), Elizabeth Atieno (Wadadia), Annette Kundu (Eldoret Falcons), Lilian Awuor (Vihiga Queens);

Mabeki – Lilian Adera (Vihiga Queens), Maureen Khakasa (Trans Nzoia Falcons), Vivian Nasaka (Vihiga Queens), Enez Mango (Vihiga Queens), Dorcas Sikobe (Oserian), Esther Nadika (Gaspo), Lucy Akoth (Mathare United Women), Lidiah Nasike (Makolanders), Lydia Akoth (Thika Queens), Stella Anyango (Gaspo);

Viungo – Myline Awuor (Vihiga Queens), Sheril Angachi (Gaspo), Cynthia Shilwatso (Vihiga Queens), Vivian Corazone (pichani na ambaye huchezea Gaspo), Yvonne Kavere (Soccer Queens), Cynthia Matekwa (Nyuki Starlets), Janet Bundi (Eldoret Falcons), Rebecca Akinyi (Oserian Ladies), Maurine Achieng’ (Vihiga Queens), Martha Amunyolete (Trans Nzoia Falcons), Bertha Omita (Kisumu All Starlets), Mwanahalima Adam (Thika Queens), Rachael Muema (Thika Queens), Elizabeth Wambui (Thika Queens);

Washambuliaji – Topista Nafula (Vihiga Queens), Tumaini Waliaula (Trans Nzoia Falcons), Mercy Airo (Kisumu All Starlets), Phoebe Owiti (Vihiga Queens), Terry Engesha (Vihiga Queens), Susan Muhonja (Trans Nzoia Falcons), Cynthia Achieng (Kisumu All Starlets), Winnie Kanyotu (Gaspo Youth), Elizabeth Katungwa (Kwale Girls).

You can share this post!

DAU LA MAISHA: Awika katika nyanja inayochukuliwa kuwa ni...

MWANAMKE MWELEDI: Kidedea katika sekta ya benki

adminleo