• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
MWANAMKE MWELEDI: Kidedea katika sekta ya benki

MWANAMKE MWELEDI: Kidedea katika sekta ya benki

Na KEYB

MWAKA 2001 aliandikisha vitabu vya kumbukumbu kwa kuwa mwanamke wa kwanza kupewa wadhifa wa Afisa Mkuu Mtendaji na Meneja Mkurugenzi wa Benki ya Diamond Trust Bank (DTB) Group.

Ni rekodi ambayo Nasim Devji anaendelea kuishikilia hadi sasa kwani hadi leo hakuna mwanamke mwingine amewahi kuhudumu katika nafasi hiyo.

Ustadi wake umezidi kudhihirika kwani chini ya uongozi wake, DTB Group imeimarika na kuwa mojawapo ya benki zinazokua kwa kasi.

Aidha, katika muda wote wa huduma yake katika benki hii, Devji ametoa mchango mkubwa katika sekta ya benki na katika harakati hizo kupokea tuzo kocho kocho.

Mwaka wa 2010, alitajwa kama mwanamke anayeongoza katika biashara barani katika tuzo za The Africa Investor, Investment and Business Leader Awards.

Mwaka wa 2011 na 2014, alipokea tuzo ya Afisa Mkuu Mtendaji wa mwaka kutoka kwa Halmashauri ya kitaifa ya inayodhibiti fedha (Capital Markets Authority).

Aidha, mwaka wa 2011 na 2013, alitambuliwa kama Afisa Mkuu Mtendaji wa mwaka katika sekta ya benki na kampuni ya Think Business Limited.

Lakini haikuwa rahisi kufika alipo kwani safari yake ilijaa changamoto. Kila wakati katika taaluma yake, alijipata akiwa mwanamke pekee miongoni mwa wafanyakazi wenza wa kiume.

Ni changamoto aliyoanza kukumbana nayo katika miaka ya themanini, ambapo alikuwa akihudumu kama mtaalamu wa ushuru katika sekta ya mafuta nchini Uingereza.

‘Haikuwa rahisi’

Wakati huo, haikuwa kawaida kuwapata wanawake wakishikilia nafasi za usimamizi katika sekta hiyo.

Lakini licha ya changamoto hizo, Devji alizidi kumakinika na kuzitumia kama jukwaa la kuimarisha uwezo wake kitaaluma.

Alijiendeleza kimasomo nchini Uingereza baada ya kukamilisha masomo yake ya shule ya upili nchini Tanzania. Alihitimu na shahada ya digrii katika masuala ya uhasibu.

Baadaye, alisomea masuala ya ushuru na kisha akafuatisha na masuala ya ushuru katika fani ya mafuta na gesi.

Mwaka wa 1996, baada ya miaka 25 akiwa ng’ambo, aliwasili nchini Kenya na kuungana na DTB Group kama mratibu wa eneo hili na mdhibiti wa fedha.

Devji ni mwanachama wa taasisi ya mahasibu nchini Uingereza (Institute of Chartered Accountants of England and Wales), chama shirika cha taasisi ya utozaji ushuru nchini humo. Vile vile, yeye ni mwanachama wa taasisi ya kitaifa ya wahudumu wa benki nchini Kenya.

Mbali na hayo, pia anahudumu kama mkurugenzi wa benki za DTB Tanzania, DTB Uganda, DTB Burundi, mashirika ya bima ya Jubilee Insurance Burundi na Diamond Trust Insurance Agency Limited.

Aidha, yeye pia ni mwanachama wa Bodi ya Hazina ya kulinda amana nchini (Deposit Protection Fund Board in Kenya).

Devji anasema kwamba ufanisi wake unatokana na bidii na imani thabiti kwamba mtu akiwa na umakini kuhusu anachofanya na kujitolea, basi bila shaka bidii yake itatambuliwa na mtu mwingine.

Anahimiza wanawake na vijana kuwa tayari kupitia magumu kwani safari hasa ikikosa changamoto, basi kiongozi huwa dhaifu.

Anapania kuwanasihi wanawake na vijana ambapo anasisitiza kwamba kila mmoja anapaswa kupewa fursa ya kujiiendeleza kitaaluma iwapo anaonyesha nia ya kufanya kazi.

Aidha anasema kwamba kama mwanamke, ili kujiendeleza katika sekta ya benki sharti udhihirishe kwamba unaweza kufanya kazi kwa umakini na bidii.

Devji anahimiza yeyote aliye na ndoto kufungia macho vizingiti vinavyomzuia asiafikie malengo yake.

You can share this post!

Harambee Starlets kuingia mazoezini Jumapili maandalizi...

Mhadhiri mtafiti wa MKU azidi kutia fora

adminleo