Makala

SIHA NA LISHE: Viungo mbalimbali na faida katika mapishi na afya kijumla

July 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MARGARET MAINA

[email protected]

Kitunguu saumu

KITUNGUU saumu ni kiungo ambacho ni maarufu kwa matumizi mbalimbali.

Kitunguu saumu hufaa katika matatizo mengi kama kusaidia kuzuia maambukizi katika utumbo na mapafu, husaidia katika uyeyushwaji wa chakula, huzuia kuharisha na pia hupunguza fangasi za kinywani.

Ni muhimu pia kukabiliana na maambukizi katika koo.

Kitunguu saumu kinaweza kutumika katika mapishi ya chakula, chai au kinywaji chochote.

Tangawizi

Tangawizi ni kiungo ambacho kinatokana na mizizi ya mmea wa tangawizi.

Kiungo hiki mara nyingi hutumika kikiwa kibichi au kikiwa kimekaushwa na kusagwa kuwa unga.

Tangawizi inaweza kutumika katika vinywaji vilivyochemshwa.

Pia huongezwa kwenye vinywaji vingine au kwenye chakula. Ni muhimu izingatiwe kwamba husaidia kuongeza hamu ya kula, kupunguza kutapika, kuharisha, maumivu ya tumbo na gesi tumboni.

Pia husaidia uyeyushwaji wa chakula tumboni. Mtu anapokuwa na matatizo ya mafua au flu, inashauriwa ale tangawizi au anywe maji yake.

Tangawizi. Picha/ Margaret Maina

Iliki

Iliki ni mbegu zinazotokana na mmea wa iliki ambazo hutumika kama kiungo. Mbegu hizi huweza kusagwa au kutwangwa na kuongezwa kwenye chakula au katika vinywaji. Iliki ni nzuri na husaidia kupunguza maumivu, kutapika ,Pia husaidia uyeyushwaji wa chakula na huongeza hamu ya kula.

Mdalasini

Mdalasini ni kiungo ambacho unaweza kusaga kabla ya matumizi au hata kitumike bila kusagwa. Vilevile mdalasini huongezwa kwenye chakula au katika vinywaji vilivyochemshwa au hata vikiwa baridi.

Mdalasini husaidia kupunguza matatizo kama mafua au flu, vidonda vya kinywani na hata fangasi za ngozi.

Vilevile kiungo hiki huongeza hamu ya kula, pia husaidia kupunguza baadhi ya matatizo katika mfumo wa chakula, kutapika au kuharisha. Kinywaji kilichochemshwa chenye mchanganyiko wa mdalasini na tangawizi kinaweza kutuliza kikohozi.

Giligilani

Giligilani ni aina ya kiungo ambacho majani na mbegu zake hutumika kama kiungo katika mapishi ya vyakula mbalimbali kama nyama, supu au mchuzi.

Kiungo hiki husaidia kuongeza hamu ya kula na kupunguza gesi tumboni. Pia husaidia kuzuia maambukizi ya bakteria na fangasi.

Binzari / Manjano

Mizizi ya binzari hukaushwa, husagwa na kisha kutumika kutengeneza unga wa binzari ya manjano ambao hutumika kama kiungo cha chakula.

Vilevile binzari mbichi inaweza kutwangwa na kutumika kwenye mapishi mbalimbali.

Binzari ikitumiwa katika chakula, hukifanya kuwa na rangi ya njano.

Binzari inaweza pia kutumika kwenye mapishi ya wali au vyakula vingine vya nafaka na vilevile kwenye mchuzi au maharagwe kuyapa ladha ya kipekee.

Manjano. Picha/ Margaret Maina