• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 10:55 AM
Wahatarisha maisha kuuzia bidhaa karibu na mabomba ya mafuta

Wahatarisha maisha kuuzia bidhaa karibu na mabomba ya mafuta

SAMUEL BAYA na ERICK MATARA

WAFANYIBIASHARA wa soko Mjinga linalopatikana katika mtaa wa Kaptembwa, viungani mwa mji wa Nakuru wanahatarisha maisha yao kwa kufanya biashara juu ya bomba la mafuta la kampuni ya KPC.

Vilevile ni katika eneo hilo ambapo nguzo za umeme wenye nguvu nyingi zinapitia juu yao hivyo basi kuzidi kuhatarisha maisha yao.

Kuna jumla ya wafanyabiashara wapatao 500 ambao hufanya biashara katika eneo hilo licha ya hatari ambayo inawakabili endapo kutakuwa na moto katika eneo hilo.

Katika eneo hilo biashara nyingi ikiwemo vibanda vya kuuzia mboga, nguo na vifaa vya kielektroniki vimekuwa vikiuzwa hapo licha ya hatari hiyo.

Baadhi ya wafanyabiashara tulioongea nao walikiri kwamba wako katika hatari lakini hapo ndipo mahali pekee kwa kufanyia biashara.

Aidha wauzaji hao walisema wako tayari kuhamia maeneo mengine lakini endapo watatengewa maeneo ya kufanyia biashara zao.

Wakati Taifa Leo ilipokutana na Bi Hellen Karonje, katika kibanda chake, mama huyo alisema hana mahali pengine pa kwenda ili kuitafutia riziki familia yake.

Aidha mfanyabiashara huyo ambaye amefanya kazi kwa miaka kumi katika eneo hilo alisema ari ya kuitafutia familia yake ndiyo iliyomfanya kufika katika eneo hilo na kuweka kibanda cha chakula.

“Hatuwezi kukataa kwamba tunahatarisha maisha yetu ila hapa ndipo eneo pekee ambako tunaweza kuendeleza biashara hii. Tukiondoka hapa bila eneo lengine kupatiwa, familia zetu zitapata shida,” akasema Bi Karonje.

Mfanyabiashara mwengine Bi Mary Wanjiku, ambaye pia huuza chakula katika soko hilo alisema kuwa ni wazi eneo hilo ni hatari lakini hawana namna ila tu kuendelea mbele na biashara.

“Maisha sio rahisi na kwa sababu tunataka kuzilisha familia zetu, hatuna budi kurauka kila asubuhi kuja hapa licha ya hatari ambayo inatukabili,” akasema Bi Wanjiku.

Mbali na hatari ya mlipuko wa moto katika soko hilo, Taifa Leo iligundua kwamba wafanyabiashara hao hawana vyoo hivyo basi kuhatarisha mkurupuko wa magonjwa.

Kulingana na msimamizi mkuu wa usalama katika kampuni ya KPC eneo la Nakuru Bw Walter Ochieng, wachuuzi hao hawatakikani karibu na mabomba hayo ya mafuta.

You can share this post!

Wengi hawana ujuzi wa kazi licha ya kufuzu vyuoni –...

Mahakama yatoa agizo nyama iharibiwe

adminleo