MAPISHI: Jinsi ya kupika maini ya ng’ombe
Na MARGARET MAINA
Muda wa kuandaa: Dakika 10
Muda wa kupika: Dakika 20
Walaji: 3
Vinavyohitajika
maini ya ng’ombe kilo 1
nyanya 4
kitunguu maji 1
karoti 1
pilipili mboga za rangi tofauti
juisi ya limau vijiko 3
chumvi
majani ya giligilani
mafuta ya kupikia
Utaratibu
Anza kwa kutayarisha maini. Ondoa ngozi ya juu ya ini ambayo huwa ngumu.
Osha kisha kata vipande kwenye ukubwa unaopenda.
Nyunyuzia juisi ya limau kwenye vipande vya ini na kisha weka chumvi.
Changanya vizuri ili vipande vichanganyike sawia.
Andaa viungo kwa kuosha na kuvikata vipande vidogo; nyanya, pilipili mboga, karoti na vitunguu.
Weka mafuta ya kupikia kwenye sufuria, au kikaangio unachotumia kupikia maini.
Weka maini. Yakaange hadi yaive kama dakika 10.
Weka kitunguu, koroga na uache viive vizuri.
Weka pilipili mboga na karoti. Koroga kwa dakika tano.
Weka nyanya huku ukikoroga; punguza moto uwe wa wastani.
Baada ya dakika 10 unaweza kuepua kwa kuwa nyama imeiva.
Pakua kwa wali,chapati,viazi vilivyobondwa au chochote ukipendacho na ufurahie