Habari

Amuua babake kwa kumkata kichwa, ajitetea alidhani ni mbuzi!

July 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA MARY WANGARI

WAKAZI Nanyuki wameelezea hofu kuhusu ongezeko la visa vya mauaji eneo hilo baada ya mwanamme mwenye umri wa miaka 29 kumuua babake kwa kumkata kichwa akidai alidhani alikuwa anachinja mbuzi katika kisa kilichowaacha wengi vinywa wazi.

Dennis Mwangi alimvamia na kumkata kichwani babake mzazi Peter Ndegwa mwenye umri wa miaka 59 mnamo Jumanne adhuhuri, wakiwa nyumbani kwao eneo la Kimathi Estate karibu na shule ya Msingi ya Nanyuki, Kaunti ya Laikipia.

Kulingana na wakazi walioshuhudia kisa hicho cha kushtua, mshukiwa alimkata kichwa babake aliyekuwa akiugua kwa muda, akakitia kwenye ndoo na kisha kuanza kuzunguka nacho mjini Nanyuki.

Ajabu ni kwamba hata baada ya kumuua babake kinyama, Mwangi hakutoroka na alipoulizwa kiini cha kufanya hivyo alisema alidhani alikuwa akimchinja mbuzi hali iliyoashiria huenda alikuwa akikabiliwa na matatizo ya kiakili.

Maafisa wa polisi walifika na kumtia mbaroni mshukiwa huku mwili wa mwendazake ukipelekwa katika Mochari ya Rufaa ya Nanyuki.

OCPD wa Laikipia Mashariki Bw Kizito Mtoro alithibitisha kisa hicho akisema maafisa wa polisi hawakuweza kubainisha nia ya mauaji hayo mara moja.

Aliongeza kwamba uchunguzi unaendelea huku mshukiwa akisubiri kufikishwa mahakamani ili afanywe mashtaka.

Marehemu alikuwa mfanyabiashara maarufu na alimiliki duka katika jumba Joskaki mjini Nakuru. Aidha, alikuwa mwanasiasa aliyewania kiti cha useneta kaunti ya Murang’a katika uchaguzi mkuu uliopita 2017.

Kulingana na wakazi, kisa hiki ni mojawapo tu wa misururu ya visa vya kutatanisha ambavyo vimekuwa vikitendeka katika kaunti hiyo huku wakielezea hofu na wasiwasi wao kuhusu ongezeko la visa vya mauaji katika eneo hilo.

“Nanyuki kumekuwa na visa vingi vya kutatanisha. Tunahitaji maombi,” anasema Bi Enny Shii mkazi wa Nanyuki.

Mwezi uliopita, mwanamme mmoja aliripotiwa kumuua mamake katika kijiji cha Matanya kilicho karibu na mpaka wa Kabanga na Kamangura. Katika mwezi huo huo eneo la Daiga, mwanamme mmoja aliripotiwa kumuua mpenzi wake ambaye pia alikuwa mke wa mtu.

Taifa Leo Dijitali inaomba radhi kwa wasomaji kuhusu maelezo ya kutisha na kuogofya ya jinsi mshukiwa ameripotiwa kutekeleza mauaji hayo.