• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:03 AM
Loyanae aongoza Wakenya kutangaza ubabe Seoul Marathon

Loyanae aongoza Wakenya kutangaza ubabe Seoul Marathon

Na GEOFFREY ANENE

KENYA imenyakua taji la wanaume la mbio za Seoul Marathon kupitia Wilson Loyanae na kupoteza lile la wanawake nchini Korea Kusini, Jumapili.

Loyanae, ambaye aliwahi kupigwa marufuku kwa matumizi ya dawa za kusisimua misuli Februari mwaka 2013, aliibuka mshindi kwa saa 2:06:57 jijini Seoul.

Bingwa huyu wa mwaka 2012, 2015 na 2016 aliwalemea kasi wapinzani wake wa karibu zikisalia kilomita tano. Alifuatwa unyounyo na Wakenya wenzake Mark Korir (2:07:03), Benson Kipruto (2:07:11), Marius Kimutai (2:07:45) na Felix Kipchirchir (2:07:57) katika usanjari huo.

Mkenya Margaret Agai, ambaye alikuwa akitetea taji la wanawake, alitupwa nafasi moja chini mwaka 2018. Alimaliza nyuma ya Muethiopia Damte Hiru aliyeshinda kwa saa 2:24:08. Agai alikamilisha sekunde 22 nyuma (2:24:30). Mkenya Monica Jepkoech (2:24:31) na Muethiopia Mulu Seboka (2:25:01) waliridhika katika nafasi za tatu na nne, mtawalia.

Wakimbiaji watano wa kwanza walizawadiwa Sh8 milioni, Sh4 milioni, Sh2 milioni, Sh1 milioni na Sh708,568, mtawalia.

You can share this post!

Bao moja labandua Gor nje ya Klabu Bingwa Afrika

‘Flash’ afikia rekodi ya Mehta kwenye Safari...

adminleo