Makala

ULIMBWENDE: Jinsi ya kutunza nywele kwa gharama ndogo

July 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MARGARET MAINA

[email protected]

WATU wengi siku hizi wameweka nywele zao asilia (natural hair).

Kwa wale wanaofikiria kuanza kuwa na nywele asilia, wanaweza kuzingatia utaratibu na mambo yafuatayo ili kukuza nywele asilia kwa haraka zaidi.

Unazifahamu nywele zako vizuri? Una nywele za aina gani? Zina sifa gani? Unafaa kuzitunza namna gani?

Usafi wa ngozi ya nywele na nywele zenyewe

Ili nywele ziwe na afya, inafaa ngozi ya kichwani nayo iwe safi. Ukitaka nywele zako zisidumae, zioshe vizuri.

Ngozi safi ya nywele itasababisha nywele kupata njia ya kujitokeza nje kwa urahisi.

Unapoziacha chafu, ule uchafu unaziba matundu ya nywele zako na kuzuia njia, kama ambavyo matundu ya uso yakiziba unapata chunusi.

Linda unyevu wa nywele zako

Kila mtu akisikia kiu hunywa maji. Nywele zako zinahitaji kulindwa zisisikie kiu. Unapoziosha, yale mafuta asilia ya kuzilinda huondoka na uchafu.

Nywele zinabaki zikiwa na udhaifu fulani kwa kuwa haziwezi kushikilia hayo maji yaliyopo vizuri, na zikikauka zinakuwa kavu sana.

Kwa nywele ambazo ni nyepesi na chache, pia kuna bidhaa za kuzisaidia ziweze kutunza vizuri unyevu na hivyo kuwa na afya nzuri.

Mafuta ya kupaka kichwani

Haya mafuta ni ya muhimu mno. Mafuta ya nazi yanaweka afya nzuri kwa nywele aina nyingi.

Pia mafuta kama ya mizeituni na ya tea tree ni muhimu.

Kuzichambua vizuri kabla ya kuchana

Uwe mkarimu na mwenye subira kwa nywele zako. Unapaswa kizichambua nywele zako kwa mikono taratibu wakati mwingine unaweza kuzilowesha na maji kabla ya kuzichana kwa chanuo.

Usizisumbue mara kwa mara na usuke mitindo ya kuzitunza zikue

Kama unataka zikue haraka, usizisumbue nywele zako sana.

Unaweza ukasuka mitindo mizuri ukakaa nazo wiki nzima au kadri zitakavyodumu au upunguze kuzichana mara kwa mara lakini utafute siku kama wikendi uzichambue taratibu kwa vidole.

Kuchana mara kwa mara kiasi cha kupindukia husababisha zikakatika au ziwe nio za kuanguka.

Cha kuzingatia

Punguza matumizi ya vitu vya moto kwenye nywele zako kama pasi ya nywele na vinginevyo.