• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:45 AM
AKILIMALI: Kuza mboga asili aina ya ‘saga’ soko likutafute

AKILIMALI: Kuza mboga asili aina ya ‘saga’ soko likutafute

Na SAMMY WAWERU

BI Florah Wambui wakati akianza ukulima, hakuwa na soko tayari la mazao.

Wataalamu wa masuala ya kilimo na uchumi hushauri kabla mkulima kukuza mimea, wanapaswa kufanya utafiti wa jinsi ya kupanda, matunzo na gharama yake, pamoja na soko.

Kulingana na mtaalamu Harry Thuku, ukianza ukulima bila ufahamu wowote, kilele chake kitakuwa mahangaiko.

Anasema haja ipo kufanya ziara kwa wakulima waliofanikiwa na waliobobea ili kujifunza mambo kadha wa kadha.

Mdau huyu anaendelea kueleza kwamba pembejeo yaani; mbegu, mbolea na dawa dhidi ya wadudu na magonjwa, ni vigezo mkulima chipukizi anapaswa kupata ufahamu wake kikamilifu.

“Mitandao ya kijamii, na wakulima waliofanikisha shughuli za kilimo, hadithi zao zitamhami kwa maarifa. Pia atajua namna ya kukiendesha.

“Wakati akiendelea kutunza mimea anayokuza, ni muhimu aanze kutafuta soko la mazao ili asiishie kuhangaika,” afafanua Bw Thuku.

Soko

Florah Wambui alipoanza kilimo mwaka 2017, alizingatia baadhi ya vigezo hivyo lakini kile cha soko hakikumtia wasiwasi.

Mama huyu anasema azma yake ilikuwa kuafikia matamanio kuhusishwa na shughuli za kilimo.

“Nililelewa katika familia iliyoenzi kilimo kaunti ya Kirinyaga. Nilipokuja Nairobi, nilijishughulisha na kazi za kuajiriwa ingawa nilihisi sikuwa kamilifu bila kulima,” anaelezea Wambui.

Kwa sasa Wambui ambaye ni mama wa watoto wanne, ana kila sababu ya kutabasamu baada ya kukirejelea.

Bi Florah Wambui, mkulima wa mboga asili aina ya saga eneo la Mwiki, Nairobi. Picha/ Sammy Waweru

Ni mmoja wa wakulima tajika katika mashamba ya eneo la Mwiki, Nairobi, ambapo hukuza mboga asili kama mnavu, mchicha, saga na kansella.

Kulingana naye ni kuwa saga ni miongoni mwa mboga za kienyeji ambazo mkulima hatahangaika kutafuta soko kwa sababu ya mahitaji yake.

“Saga ni kama mahamri moto sokoni. Wateja hujia mboga hii shambani,” anasema.

Hii ni kutokana na faida zake kiafya, kando na mapato kwa mkulima.

Katika orodha ya mboga za kienyeji, utafiti unaonesha kwamba saga ina faida tele kiafya ikilinganishwa na zingine.

Imesheheni Beta-carotene, Vitamini C na A.

Saga pia ina ukwasi wa madini ya Calcium, Magnesium, Phosphorous na Iron.

Aidha, inakadiriwa kuwa na asilimia tano ya Protini na asilimia sita Wanga.

Kulingana na Bi Florah majani na sehemu yake ya matawi huvunwa na kupikwa pekee au kwa kuchanganya na mboga zingine. “Pia hupondwapondwa na kuchanganywa na matunda kuunda juisi,” anaeleza mkulima huyu.

Baadhi ya watu hupika mboga hii ya kienyeji na kuichanganya na maziwa au siagi yake, ambapo huacha mlaji akidondokwa na mate kwa ajili ya ladha yake.

Saga inaaminika kuimarisha uwezo wa kuona, kukabili shida za kusokotwa na tumbo na Kifua Kikuu. Katika jamii ya Kalenjin, mboga hii aghalabu hulishwa wavulana waliopashwa tohara, wakiendelea kupata nafuu ya kisu cha ngariba.

Maeneo ya Kisii, Nyamira, Kisumu, Uasin Gishu na Tharaka Nithi, ndiyo tajika katika uzalishaji wa saga.

Kilimo chake kinafanikishwa maeneo yenye kiwango cha joto nyuzi 18-25.

Veronica Kirogo, mtaalamu, anasema saga inahitaji udongo tifutifu, au tifutifu uliochanganyika na kichanga.

“Udongo usiwe wa kutuamisha maji,” anasisitiza Bi Kirogo.

Kilo mbili za mbegu ya saga hugharimu Sh1, 200 kwa wanaozikuza mara ya kwanza. Kwa wenye uzoefu, hawahitaji kuzinunua kwani husubiri misaga ikomae ili kupata mbegu.

Kulingana na Florah Wambui shamba linapoandaliwa, saga hazina utaratibu wa upanzi. Hazihitaji miche, kwani mbegu zake hupandwa moja kwa moja.

Mkulima huyu huzichanganya na mboga zingine kisha anamwaga tambarare. Hunyunyuzia maji kwa jenereta. Wataalamu wa kilimo hata hivyo wanashauri haja ya kuzingatia taratibu za upanzi kitaalamu.

Wanahimiza umuhimu wa kuandaa mashimo au mitaro, ili kupata mazao bora na mengi.

“Haipaswi kuchanganywa kulima na mboga zingine kwa wakati ule mmoja. Hilo huleta ushindani wa lishe; maji na mbolea,” anaeleza Veronica Kirogo.

Wambui anatetea mkondo wake akitoa sababu kwamba ‘mashamba Nairobi ni haba’, hivyo basi anaweza kukuza mboga mbalimbali.

Saga huanza kuvunwa mwezi mmoja baada ya upanzi.

Kuna wanaong’oa misaga, hususan kupanda mingine au kufanya mzunguko wa mimea.

Hata hivyo, Wambui huendelea kuvuna yake kwa muda wa karibu miezi mitatu mfululizo.

Ekari moja iliyotunzwa vizuri inaweza kuzalisha karibu tani 20 za mboga ya saga. Kilo moja haipungui Sh30.

Ingawa ni nadra saga kushambuliwa na wadudu, Vidukari na Vithiripi ndio changamoto kuu kwa mboga za kienyeji.

Pia, magonjwa yanayoathiri mboga hushuhudiwa mkulima asipotilia maanani suala la mzunguko wa mimea.

Unahimizwa kupata maelekezo ya mtaalumu kwa ajili ya dawa bora kupulizia.

Hali kadhalika, kuwepo kwa mbegu ya hadhi ndiyo changamoto inayokumba wakuzaji wa saga. Suala la kurejesha mbegu zilizokomaa katika shamba lilelile zilikokuziwa hushusha kiwango cha mazao.

  • Tags

You can share this post!

Jaji Jessie Lesiit adinda kujiondoa kusikiliza kesi ya...

Mchakato wa kura ya maamuzi ‘kuiva’

adminleo