Padri mlevi asababisha mauti ya mhubiri na mkewe
Na WAWERU WAIRIMU
WATU watatu wa familia moja, akiwemo mhubiri na mkewe, walifariki Jumamosi asubuhi baada ya kuhusika kwenye ajali ya barabarani eneo la Maili Saba katikati ya Isiolo na Meru.
Inasemekana kwamba, ajali hiyo ilitokea wakati gari la pasta huyo liligongana na gari la padri ambaye polisi walisema alikuwa mlevi. Kulingana na polisi, gari walilokuwa wakisafiria liligongana ana kwa ana na gari lililokuwa likiendeshwa na Padri wa Kanisa Katoliki kutoka Isiolo jana asubuhi
Mchungaji huyo, mkewe na abiria mwingine waliokuwa wakielekea Mwingi kutoka Isiolo kuhudhuria mazishi ya jamaa yao, walifariki papo hapo huku mwana wa mchungaji akilazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Isiolo akiwa na majeraha.
Kulingana na Kamanda wa Polisi eneo la Buuri, Bw Joseph Asugo, kasisi huyo aliyekuwa akielekea Isiolo aliendesha gari katika upande usiofaa na kugonga gari la mchungaji na kisha akatoweka.
Bw Asugo alieleza Taifa Jumapili kwamba inashukiwa Padri huyo alikuwa mlevi.
“Ni abiria mmoja tu wa gari lililokuwa likielekea kwenye mazishi aliyenusurika na amelazwa hospitalini akiwa katika hali mahututi,” alisema Bw Asugo.
Taifa Jumapili ilifahamu kwamba kasisi huyo na mtu mwingine aliyekuwa katika gari lililosababisha ajali walinusurika wakiwa na majeraha madogo na wakatibiwa katika hospitali moja ya kibinafsi eneo hilo.
“Kasisi na mseminari aliyekuwa katika gari hilo baadaye walikimbizwa katika hospitali iliyo karibu na wakatibiwa kwa majeraha madogo,” duru ziliambia Taifa Jumapili.
Baada ya kutibiwa, wawili hao walitoroka na hadi wakati wa kwenda mitamboni jana jioni hawakuwa wamepatikana.
Magari yote mawili yalivutwa hadi kituo cha polisi cha Subuiga, Meru. Jana, waumini wa kanisa la African Inland Church (AIC) Isiolo waliomboleza kifo cha pasta wao na mkewe wakisema ni cha huzuni.
“Tuna huzuni kwamba tumempoteza pasta wetu na mkewe wakati mmoja. Nilikuwa nao jana (Ijumaa) na wakaniambia wangesafiri leo (jana Jumamosi),” alisema muumini ambaye aliomba tusitaje jina lake.
“Tumepoteza mtumishi mashuhuri wa Mungu na tunaomba Mungu afariji familia yake na kuipatia amani wakati huu mgumu,” alisema muumini mwingine Bw Charles Kamau.
Bw Asugo aliwahimiza waendeshaji wa magari kuzingatia sheria za trafiki ili kuepuka ajali.
“Watumiaji wote wa barabara wanapaswa kutii sheria za trafiki ili tusipoteze maisha,” alisema. Miili ya watu hao watatu ilipelekwa katika Mochari ya Hospitali ya Rufaa ya Isiolo.