• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 1:15 PM
GASPO Women wajiahidi kumaliza ndani ya tatu bora

GASPO Women wajiahidi kumaliza ndani ya tatu bora

Na JOHN KIMWERE

TIMU za michezo huanzishwa kwa madhumuni tofauti ikiwamo kukuza talanta za chipukizi angalau wakomae na kuibuka kati ya wachezaji wa kimataifa miaka ijayo.

Taifa hili limefurika timu nyingi tu za wanaume na wanawake katika kila kona ambazo zimejitwika jukumu la kunoa makucha ya wahusika huku wakidhamiria kutinga hadhi ya kutumia talanta zao kujikimu kimaisha.

”Tulianzisha GASPO Women ili kusaidia wasichana kutambue kipaji chao na kukinoa bila kuweka katika kaburi la sahau kutafuta mbinu za kuwainua kimaisha,” meneja wake, Edward Githua anasema na kudai kuwa wamepania makubwa ndani ya miaka michache ijayo.

GASPO Women imeibuka kati ya vikosi vinavyotifua vumbi kali kwenye mechi za Soka la Wanawake la Ligi Kuu ya Kenya (KWPL) msimu huu. Timu hii iliasisiwa mwaka 2006 ingawa inashiriki ngarambe hiyo kwa mara ya pili, baada ya kucheza Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza kwa miaka minne.

GASPO Women ya kocha, Isaac Mwathe ilionekana kuja kivingine kwenye kipute hicho mwishoni mwa mechi za mkumbo wa kwanza licha ya kuibuka ya tano msimu uliyopita.

Mchezaji wa GASPO Women, Wincate Kaari (kulia) akionyesha weledi wake wakati kikosi hicho kilipokutanishwa na Kisumu Allstars kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Wanawake ya Kenya (KWPL) katika uwanja wa Ruiru Stadium mjini humo. Picha/ John Kimwere

”Tayari timu zinazoshiriki mechi za msimu huu zimeonyesha zimejipanga kupigania taji hilo kwa udi na uvumba,” meneja huyo anasema na kuongeza kuwa wamepania kujituma kiume wakilenga kumaliza kati ya tatu bora.

Anakiri kuwa kamwe haitakuwa mteremko kutimiza azimio hilo. Anadokeza kuwa vipusa wake wanakabiliwa na shughuli nzito mbele ya mahasimu wao ikiwamo Trans-Nzoia Falcons, Thika Queens, Kisumu Hot stars na mabingwa watetezi Vihiga Queens kati ya zingine.

”Licha ya upinzani tunaotarajia msimu huu nina imani tukimakinika tutafanya vizuri,’ nahodha wake, Winnie Mugechi alisema na kutoa mwito kwa kikosi chake kutolaza dimbani.

GASPO Women hufadhiliwa na rais wa taifa hili, Uhuru Kenyatta lakini haijafanikiwa kujika vizuri.

”Tunahitaji gari la kusafirisha wachezaji wetu maeneo ya mbali kushiriki mechi za ligi na kirafiki pia linaweza tuletea fedha kupitia kulikodisha. Aidha tunahitaji uwanja wetu maana nyakati zingine viwanja nyingine hukosekana baada kukodishwa kwa shughuli zingine,” alisema.

Ofisa wake mkuu, Salome Njeri anasema wamo kwenye mchakato wa kuingia dili na kampuni ya maziwa ya Tuzo mpango unatazamiwa kuweka wachezaji hao vizuri ili wawe wakipokea posho kila mwezi.

”Tunadhamiria kuanzisha miradi ya kuchuna fedha ili kusaidia wasichana wa kikosi chetu kujikimu kimaisha,” ofisa huyo alisema huku akitoa shukrani za dhati kwa rais wa Kenya kwa kuwashika mkono kwenye juhudi kukuza wanasoka wa kike mashinani.

GASPO Women inajumuisha: Winnie Mugechi (nahodha), Linda Nanjala, Vivian Komulo(naibu wa nahodha), Lavyne Anyango, Emily Andayi, Madeline Otieno, Nainagwe Mwaipopo, Wincate Kaari, Elizabeth Wambui na Mary Wairimu.

Pia wapo Teresia Lundu, Lyssette Anyango, Vivian Corazone, Sheril Angach, Purity Jepto, Lilian Akinyi, Stella Anyango, Esther Nandika, Sharon Aluoch, Quinter Atieno, Leah Cherotich na Judith Osimbo.

Meneja huyo husukuma gurudumu la timu hiyo akisaidiana na wenzake akiwamo: Faith Njeri (katibu), Caroline Ndunge (mweka hazina), Salome Njeri (ofisa mkuu) pia Elijah Kamau, Lydia Wambui, Stephen Kamau, Martin Wainaina, Elizabeth Wangui na Anastasia Wangui. GASPO Women inajivunia kushinda taji la Afrika Mashariki mara mbili kwa wasiozidi umri wa miaka 16 kwenye mechi ambazo huandaliwa nchini Tanzania.

 

You can share this post!

Karugwa yapania makubwa raundi hii

Nairobi Water yajipanga kurejea ligini

adminleo