Rotich, Thugge wafikishwa mahakamani
Na SAM KIPLAGAT
WAZIRI wa Fedha Henry Rotich na Katibu katika wizara hiyo Kamau Thugge ambao wamefikishwa katika mahakama ya Milimani jijini Nairobi, walikamatwa Jumatatu na kuzuiliwa katika seli za polisi.
Wanashukiwa kuhusika pakubwa katika sakata ya mabilioni ya ujenzi wa mabwawa ya Kimwarer na Arror.
Jumatatu, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji aliagiza kukamatwa na kushtakiwa kwa watu 28, wakiwemo maafisa katika Wizara ya Fedha, Wizara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mamlaka ya Kuhifadhi Mazingira (Nema), Mamlaka ya Ustawishaji Kerio Valley na maafisa wengine wa mashirika ya serikali.
Rotich na Thugge ambao wana nyadhifa za juu wizarani waliingia katika mikono ya asasi za uchunguzi wa makosa ya jinai Jumatatu na wanakabiliwa na makosa ya ufisadi, matumizi mabaya ya mamlaka na kujihusisha na vitendo visivyofaa katika matumizi ya fedha za umma, miongoni mwa mengine.
Wanatuhumiwa kupanga njama ya kuiba kati ya Sh17 bilioni na Sh19 bilioni.
Kulingana na DPP Bw Haji, maafisa aliotaja Jumatatu wakiongozwa na Bw Rotich wanafaa kuondoka afisini mara watakapofunguliwa mashtaka.
“Ni lazima waondoke afisini. Hawa si magavana. Nitamwandikia barua Mkuu wa Utumishi wa Umma mara moja. Sheria inahitaji ukishtakiwa na ujibu mashtaka sharti uondoke. Hata katika mataifa ya nje huo ndio mwelekeo,” akasema Bw Haji.
Wakati sakata ya mabwawa ilifichuliwa, Rais Uhuru Kenyatta alikwepa shinikizo la kuwasimamisha kazi mawaziri waliotajwa akisisitiza kuwa ni lazima washtakiwe kwanza ndipo achukue hatua dhidi yao.
Alipohutubu bungeni Aprili 2019 kuhusu hali ya taifa, Rais alisisitiza lazima waliotajwa watendewe haki bali wasiadhibiwe bila ushahidi.
“Mafisadi wataadhibiwa kwa misingi ya kisheria. Hatua tutakazochukua hazitategemea jinsi watu wanavyolaumiwa kabla wasikilizwe,” akasema Rais.