KINA CHA FIKIRA: ‘Mzungumzishi’ halina mashiko kurejelea spika
Na KEN WALIBORA
NILIKUTANA na vitabu vya mwandishi Zacharia Zani enzi ya masomo yangu ya sekondari. Mfululizo wa vitabu vyake ulitawala katika mfumo wa ufundishaji wa Kiswahili katika shule za upili.
Waandishi wengine ambao vitabu vyao vilivuma ni pamoja na Clement Kabugi, Kamal Khan, Ali Attas, James Kanuri, Ruo Kimani Ruo, Gabriel R. Rwechungura, Father Kapinga.
Enzi hizo ilikuwa muhali kuhitimu masomo ya sekondari bila kukumbana na kazi za waandishi hawa mahiri waliotuwekea msingi wa vitabu vya kiada. Ilmradi tunawawia deni la shukrani magwiji hawa kwa mchango wao mkubwa katika lugha ya Kiswahili.
Je, tunamwia deni Agnes Zani kwa mchango wake katika kanzi ya msamiati wa Kiswahili? Tuna deni gani kwa Dkt Agnes Zani? Dkt Zani ni nani? Ni binti ya Mzee Zachariah na Mama Teresa Zani.
Aidha ni seneta maalumu wa chama cha ODM katika bunge la Seneti.
Hili la kuwa seneta, yaani mwanasiasa si dogo.
Hili la kuwa mtoto wa marehemu Zacharia na Teresa Zani ni kubwa zaidi. Au hilo ni dogo?
Waswahili husema “mwana wa mhunzi asiposana huvuvia.”
Je, Dkt Zani ameondokea kusana au kuvuvia? Katika hali dhanifu tungemtarajia mtoto wa gwiji wa Kiswahili kufuata nyayo za babaye na mamaye. Iwapo sijasema awali naomba niongeze kwamba Zachariah na mkewe Zani walikuwa wakufunzi katika chuo cha walimu cha Shanzu ambapo pia walishirikiana kuandika vitabu vya Kiswahili.
Swali la iwapo tuna deni la kumshukuru Dkt Agnes Zani linafungamana na kauli yake kwamba neno speaker la Kiingereza katika muktadha wa bunge, linapaswa kuwa “mzungumzishi.”
Kamusi zote za Kiswahili nilizozitazama hazina neno hili; si Kamusi Pevu ya Kiswahili, Kamusi Kuu, Kamusi Teule, Kamusi ya Kiswahili Fasaha wala Kamusi ya Kiswahili Sanifu.
Labda Kamusi zijazo au matoleo mapya ya kazi zilizoko. Kwamba Kamusi zilizoko hazina neno hili si kosa. Iwapo nakisia vizuri, (na mara nyingine mimi hukosea), neno hili halijapata kutumiwa, au kama limetumiwa halijapata ukubalifu mpana wa jumuiya ya wataalamu.
Hata hivyo, Dkt Zani ni mtoto wa wataalamu ambao wote wametuacha mkono, (Zacharia kafariki mwaka 2002 na Teresa kafa mwaka 2014).
Iwapo ni wazee wake wangalikuwa ndio waliotuundia au kutupendekezea “mzungumzishi” tungalikuwa na wajibu wa kusikiliza kwa makini. Lakini huyu ni Zani mwanasiasa na mwanasosholojia, sasa tufanyaje?
Kuna wale wanaosema kuwa lakini wanasiasa huchangia kanzi ya maneno.
Achia mbali gavana wa Pokot Magharibi Lonyangapuo aliyetuletea “kijana fupi nono round.”
Sarufi yake yenye kona inamweka nje ya wanaoweza kufikiriwa kuwa wachangiaji wa maendeleo ya Kiswahili.
Anafaa tu kwenye vipindi vya machale kama Inspekta Mwala na Churchill Live.
Mfano madhubuti ni kama vile ya Mwalimu Nyerere aliyetuletea neno “ng’atuka” (la Kizaramo) naye Jomo Kenyatta akatuletea “Harambee” (upotoshaji wa neno halumbe halumbe).
Vyovyote iwavyo “mzungumzishi” halinikai sawa.