KIU YA UFANISI: Kinyozi kwa miaka 15 na bado kazi yamridhisha
Na CHARLES ONGADI
NI mita hamsini tu kutoka steji ya matatu ya Shanzu, Mombasa, ndiko kiliko kibanda cha Nyaramba Kinyozi kinachovuma sana kwa unyoaji nywele.
Hapa tunamkuta Isaack Auta, kinyozi stadi kutoka Kaunti ya Nyamira, Kisii, akimhudumia kwa makini mmoja kati ya wateja wake wakuu.
Ijapo baadhi ya vijana wanaochipuka huibeza kazi hii kuwa isiyo na pato la kutosha kuwakimu kimaisha, kwa Auta anaipenda kazi hii na kuifurahia kila anapoifanya.
“Ni kazi ambayo napenda na naifanya kwa ghera kutokana na mapato mazuri inayoniletea,” asema Auta katika mahojiano na Akilimali majuzi.
Ni kazi ambayo Bw Auta, 34, ameifanya kwa kipindi cha miaka 15 iliyopita na imeweza kukithi baadhi ya mahitaji yake muhimu maishani. Kulingana na Auta, mara baada ya kukamilisha masomo yake ya darasa la nane, alijiunga na shule ya upili ya Enkinda eneo la Nyamira.
Lakini mara alipofika kidato cha pili, mambo yalimtumbukia nyongo baada ya wazazi wake kushindwa kumlipia karo hivyo kulazimika kuacha shule. Alijipiga moyo konde na kuamua kuyoyomea mjini Mombasa kusaka jinsi ambavyo angeweza kukwamua familia yake kutoka kwa maisha ya uchochole.
Mara baada ya kuwasili Mombasa alifanyafanya vibarua vya hapa na pale kabla ya kuajiriwa na hoteli maarufu ya Whitesands Beach kuhudumu katika jikoni. Hata hivyo, baada ya kufanya kazi kwa muda wa miaka miwili, mambo yalimwendea tenge na kujikuta akipigwa kalamu na kuamua kuingilia kazi ya ujenzi.
“Nilifanya kazi ya mjengo na zingine ngumu ngumu kwa miaka mitatu nikisaka mtaji kuanzisha biashara,” asema Auta. Baada ya kipindi hicho, alifanikiwa kukusanya kiasi cha Sh7,000 na kuamua kufungua kibanda cha kunyoa mwaka wa 2004.
Auta anakiri kupitia changamoto kibao katika miezi ya kwanza katika kazi hii lakini hali ilibadilika na kuwa shwari.
“Nilijikaza na kujifunza kunyoa aina tofauti ya staili hasa wanazopenda vijana na hata wazee wenye umri tofauti na kwa hili nikajipatia wateja kila uchao,” aeleza Auta.
Kulingana na Auta, kinachomwezesha kupata wateja kibao kila siku ni bei yake nafuu kwa wateja wake ambapo kwa kila staili analipisha Sh50 kwa kichwa.
Bei hiyo huwa ni nafuu kwa wateja wake wengi ambao hufika kunyolewa katika kibanda hiki kutoka umbali wa mji wa Mtwapa, Bombolulu na Utange.
Wafanyakazi katika hoteli za kitalii
Wateja wake wengi pia ni wafanyakazi katika hoteli za kitalii zilizoko eneo la Shanzu na Bamburi na pia wanafunzi wa Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Shanzu wanaomiminika kila wikendi kunyolewa.
Wakati kazi inaponoga hasa nyakati sherehe za Krismasi ama Iddi, anatia kibindoni kitita cha Sh3,000 kwa siku huku wakati wa kusi (wateja wachache) huenda nyumbani na kati ya Sh1,000 hadi 1,200.
Kulingana na Auta, ameweza kubadilisha maisha yake maradufu akisema kutokana na kazi yake ya kinyozi ameweza kujijengea nyumba yake anayoishi mbali na kufanya maendeleo madogo madogo huko mashambani, Nyamira.
Anakiri kwamba kazi ya kinyozi haina hasara ila tu kama utaifanya kwa umakini, uaminifu, ustadi na bila kukata tamaa.
Anawashauri vijana kutokata tamaa kimaisha bali siri kuu ni kujituma bila kuchoka katika kutafuta maisha ya siku za baadaye.
“Jipange na ulicho nacho na wala usisubiri unachoahidiwa na silaha yako kuu ni kujiamini na bidii. Tusisubiri serikali itusaidie bali tutumie vyema tulicho nacho mkononi,” ashauri Auta.
Auta anafichua kwamba ananuia kuanzisha kituo kingine cha kunyoa katika mtaa wa Bombolulu ili kuweza kukithi matakwa ya baadhi ya wateja wake wanaoishi huko.