Habari

Mswada wa kuongeza idadi ya wanawake katika bunge warejeshwa tena

July 25th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE Mwakilishi wa Wanawake wa Uasin Gishu, Bi Gladys Shollei amefufua mchakato wa kuhakikisha uwepo wa usawa wa kijinsia bungeni kwa kudhamini mswada unaopendekeza kubuniwa kwa nyadhifa 176 zaidi zitakazoshikiliwa na wanawake.

Mswada huo wa marekebisho ya Katiba hata hivyo unapendekeza kufutiliwa mbali kwa nafasi 47 za Wabunge Wawakilishi wa Wanawake, ishara kwamba sharti uidhinishwe na Wakenya katika kura ya maamuzi.

Mswada huo ambao pia unataka kuondolewa kwa nafasi za uteuzi wa maseneta na madiwani zaidi kusawazisha hitaji la kijinsia uliwasilishwa katika bunge la kitaifa mnamo Jumatano.

Wakati huu kuna maseneta maalum 18 wanawake katika seneti na zaidi ya madiwani 700 maalum katika mabunge 47 ya kaunti ambao waliteuliwa na vyama vya kisiasa baada ya uchaguzi mkuu wa 2017 kwa lengo la kufanikisha hitaji la kikatiba la usawa wa kijinsia.

Mswada huo ambao unaonekana kuongeza idadi ya wanawake bungeni ikilinganishwa na wanaume umewasilishwa siku chache baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuidhinisha mswada wa marekebisho ya Katiba uliodhaminiwa na chama cha Thirdway Alliance na unaopendekeza kupunguzwa kwa idadi ya wabunge na maseneta kutoka 416 hadi 147.

Eneobunge moja

Ili kuhakikisha uwepo wa idadi tosha ya wanawake bungeni, mswada unapendekeza kuwa maeneobunge mawili katika kaunti moja, na yanayoyopakana, yatabuni eneobunge moja ambalo litatengewa wanawake.

Kwa mfano, katika kaunti kama Kakamega yenye maeneo bunge 12, maeneobunge mawili yatahitaji kuwachagua wabunge wanawake pekee. Na kwa kutumia mfumo huo ina maana kuwa kaunti kama Nairobi yenye maeneobunge 17 italazimishwa kuchagua angalau wabunge watatu wanawake.

Zaidi ya hayo,  kaunti zenye idadi ndogo ya watu na maeneobunge zitatenga angalau eneobunge moja ambako wapigakura wanachagua mbunge mwanamke pekee.

Mswada wa Bi Shollei pia unapendekeza kuwa wale watakaoteuliwa kama wabunge maalumu wawe ni walemavu na idadi yao iongezwe kutoka 12 hadi 22.

Katiba Bunge la Seneti mswada huo unapendekeza kuwa kila kaunti iwakilishwe na maseneta wawili waliochaguliwa, mmoja kutoka kila jinsia.

“Lengo la mswada huu ni kuhakikisha kuwa usawa wa kijinsia unapatikana na makundi ya watu ambao wametengwa tangu zamani, hasa walemavu, wanapata uwakilishi bunge,” akasema Bi Shollei ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya Bunge kuhusu sheria ndogo (Delegated Legislation).