Mbunge atilia shaka utawala wa Rais Kenyatta
Na WYCLIFF KIPSANG na CHARLES WASONGA
MGAWANYIKO ndani ya Jubilee ulichukua mwelekeo mpya Jumatano pale Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi alimtaka Rais Uhuru Kenyatta ajiuzulu.
Mbunge huyo ambaye ni mwandani wa Naibu Rais William Ruto aliutaja utawala Rais Kenyatta kama ambao umejaa utepetevu mkubwa kuliko tawala zilizopita.
Bw Sudi aliongeza kuwa Utawala wa Rais Kenyatta pengine ndio mbaya zaidi katika historia ya taifa hili kwa sababu “umeporomosha uchumi wa nchi.”
“Ukiona Rais ameshindwa kukutana na wabunge wa chama chake huku magavana na maseneta wakiandamana barabarani ni ishara tosha kuwa kuna shida ya uongozi. Ni kielelezo cha Rais aliyeshindwa kuongoza nchini,”akasema Bw Sudi.
Akiongea na wanahabari nyumbani kwake eneo bunge la Kapseret, katika kaunti ya Uasin Gishu, Sudi alitoa changamoto kwa Rais Kenyatta na kumtaka ampe yeye (Sudi) nafasi ya miezi mitatu pekee na ataendesha nchini vizuri kuliko yeye (Rais Kenyatta).
“Nipeni tu miezi mitatu. Ninaweza hata kumteua Moses Kuria kuwa naibu wangu na mtaona jinsi ambavyo nitaleta mabadiliko nchini. Hakuna vita dhidi ya ufisadi vinavyoendeshwa nchini. Hizi ni sarakasi za kuwafumba Wakenya macho,” akasema mbunge huyo.
“Kama kuna Rais alikuwa mzuri basi hakuwa mwingine ila Kibaki. Hii serikali ya Uhuru ni burwe kabisa!” akafoka kwa hasira.
Bw Sudi aliwatetea aliyekuwa Waziri wa Fedha Henry Rotich na aliyekuwa Katiba wake Kamau Thugge ambao wanakabiliwa na kesi za ufisadi kuhusiana mradi wa ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer akisema wawili hao wametolewa kafara tu huku washukiwa kamili wakisazwa.
“’Shida tuliyonayo ni uongozi kutoka juu. Huu mpango wa maendeleo wa Ajenda Nne Kuu umekufa na haitafaulu hata kidogo ikiwa maafisa wa serikali wataendelea kuondolewa afisini kutokana na fitina jinsi hii,” akasema.
Kwa mara ya kwanza Bw Sudi alimshauri Naibu Rais Dkt Ruto kutozika kichw chake mchangani kama mbuni bali akubali ukweli kwamba Jubilee imekufa.
“William Ruto hebu nikuambie kwamba urafiki wako na Rais Kenyatta ni feki. Mbona watu wasio na hatia wanatolewa kafara eti kwa kisingizio cha kuendeleza vita dhidi ya ufisadi?” Bw Sudi akauliza.
Aliuliza ni kwa nini sakata ya ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer inavumishwa wakati huu ilhali mradi huo ulianza mnamo mwaka wa 2014.
“Mbona inasemekana Henry Rotich sasa ni mwizi ilhali amekuwa akiongoza Hazina ya Kitaifa kwa zaidi ya miaka saba? Hii inaonyesha kuwa kuna shida kubwa katika uongozi wa Rais Kenyatta,” akasema Bw Sudi.
Jumatano, Waziri wa Leba Ukur Yatani aliteuliw kuwa Kaimu Waziri wa Fedha kuchukua mahala pa Bw Rotich.
Na wakati huo huo, Dkt Thugge alipigwa kalamu na nafasi yake ikajazwa na aliyekuwa msimamizi wa sekritarieti ya Ruwaza ya Maendeleo ya 2030 Julius Monzi Muia aliyeteuliwa kuwa Katibu wa Wizara ya Fedha.