Yabainika baadhi ya wanafunzi wa sheria KSL waliangushwa mitihani licha ya kufanya vyema
Na PETER MBURU
CHUO cha Kutahini wanafunzi wa Sheria kabla ya kuruhusiwa kufanya kazi nchini, Kenya School of Law (KSL), kimemulikwa baada ya kubainika kuwa wengi wa wanafunzi waliofeli katika mtihani wa mwaka 2018 waliangushwa bure kwani baadhi ya waliotuma maombi karatasi zao za mitihani zisahihishwe upya waliishia kufuzu.
Licha ya kuwa wanafunzi wanahitajika kulipa ada nyingi kuwezesha mitihani yao kusahihishwa upya, kati ya wachache waliolipia kuna asilimia fulani ambayo ilibainika kuwa walikuwa wamefuzu, lakini mitihani yao ikasahihishwa vibaya.
Kulingana na rekodi za chuo hicho, wanafunzi 1,505 walifanya mtihani huo Novemba 2018 katika somo la Civil Education na 1,128 kati yao wakafuzu.
Kati ya 376 ambao walifeli, 85 walilipia mitihani yao isahihishwe upya ambapo ilibainika kuwa 28 walikuwa wameangushwa wakati walifaa kuwa wamepita.
Katika somo jingine, kati ya wanafunzi 16 waliolipia kusahihishiwa mitihani yao upya, 12 walifuzu na kubainika kuwa wanne kati yao tu ndio walikuwa wamefeli.
Mwanasheria Mkuu Paul Kihara akiwa mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Masuala ya Kisheria amekiri Alhamisi kuwa uchache wa wahadhiri na watu wa kusahihisha mitihani hiyo ni mojawapo ya sababu kuu ambazo zilisababisha wanafunzi wengi kuangushwa.
Ubora
Bw Kihara alisema ni kweli usahihishaji wa mitihani hiyo haujakuwa na ubora ufaao, lakini akasema serikali iliunda jopokazi la kuchunguza changamoto zinazokumba chuo hicho ili suluhu ipatikane.
“Ni vigumu kutarajia kuwa mwalimu mmoja atasahihisha zaidi ya mitihani 800 na afanye kazi hiyo kwa ubora. Uchache wa walimu wa kusahihisha na kufundisha imekuwa changamoto kubwa,” amesema Bw Kihara.
Lakini mwanasheria huyo Mkuu amesema kuwa hali ya vyuo na taasisi za elimu nchini kutoa masomo ya kiwango duni, kuwapitisha baadhi ya wanafunzi wasiofaa kwa kuwapa alama za juu na kukosa rasilimali za kuwezesha mafunzo ifaavyo ni sababu nyingine inayofanya wanafunzi wengi kufeli.
Wabunge, hata hivyo, walishangaa baada ya kupokea habari hizo, wakieleza hofu yao kuwa huenda kuna wanafunzi wengi ambao wameangushwa bure lakini hawana la kufanya, kutokana na hali kuwa hawana pesa za kutafuta huduma za usahihishaji upya.