Habari

Maina Njenga awataka wanasiasa kutowatumia vijana kuzua vurugu za kisiasa

July 26th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANGI MUIRURI

ALIYEKUWA kinara wa kundi haramu la Mungiki, Yohanna Maina Njenga amewaonya baadhi ya wanasiasa wa Mlima Kenya dhidi ya kusajili vijana wa eneo hilo katika harakati za siasa za kuzua vurugu.

Akijitenga na uwezekano wa kuwa mshirika wa njama ya kufufua kundi la Mungiki ambalo aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, John Michuki alilivunja mwaka wa 2007, Njenga aliambia Taifa Leo hauungi kamwe harakati za kufufua kundi hilo au makundi yoyote haramu nchini.

Alisema Alhamisi kuwa badala ya serikali kuzindua harakati za kuwaandama vijana wanyonge ambao sanasana hujiingiza katika makundi hayo kwa hamu na tamaa ya hela ambazo hutolewa na wanaowasajili, “wa kuandamwa wanafaa kuwa hao wanasiasa.”

Kwa sasa, dokezi za kiusalama zinaashiria kuwa katika Mlima Kenya, kundi hilo la Mungiki linarejeshwa na wanasiasa ambao wanalumbana ndani ya mirengo ya ‘Tangatanga’ na ‘Kieleweke’ na ambapo vijana hao wanatumiwa kuvuruga mikutano ya wapinzani, hali ambayo tayari imemkumba Waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri ambaye hivi majuzi mkutano wake katika Kaunti ya Nyeri ulitibuliwa.

Njenga ambaye tangu 1987 hadi 2007 alikuwa kinara wa kundi hilo lililojulikana kwa ukatili wa mauaji, utozaji ushuru, ukeketaji wa wanawake na uvamizi wa kujeruhi aliambia Taifa Leo kuwa “sasa hakuna nafasi ya kushirikisha vijana katika miradi ya kuwapotezea maisha yao.”

Alisema kuwa anaunga mkono mageuzi ya katiba ambayo yatazingatia ujumuishaji wa vijana katika maamuzi muhimu ya kiutawala.

“Badala ya kuwaweka vijana katika hatari ya kulumbana na maafisa wa polisi, ni heri tungewaweka pamoja katika mpangilio halali wa kusaka sauti ndani ya serikali. Hakuna haja ya kuwahatarishia maisha yao katika miradi ambayo tumejaribu na tukaona haina afueni na hata haina mwelekeo katika dunia ya kisasa,” akasema.

Alisema kuwa ndani ya Mungiki alikumbana na mateso yasiyo na kifani yakiwemo kuuawa kikatili kwa mke wake, kufungwa jela na hata kujaribiwa mara kadhaa kuuawa.

“Lakini mateso haya yoye, asema, yalimleta karibu na Mungu na ikawa ni lazima ningeokoka kwani mwisho wangu ulikuwa unanukia nisingechukua hatua hiyo. Leo hii kuniambia niunge mkono vijana kuingia katika mtego wa mauti ni sawa na kunitusi,” akasema.

Alisema kuwa kwa sasa juhudi zote zinafaa kuimarishwa za kuwaongoza vijana wa taifa hili kupambana na masuala ambayo yamedadisiwa kuwa hatari kuu kwa maisha yao.

“Hatari hizo ni umaskini, ujambazi, ulevi, ukahaba na uzembe. Hayo ni masuala ambayo tunaweza tukaafikia kupitia harakati halali ndani ya mpangilio halali,” akasema.