• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
AKILIMALI: Mfugaji Limuru asema nguruwe wana faida

AKILIMALI: Mfugaji Limuru asema nguruwe wana faida

Na MARY WANGARI

NI kipi kinakujia akilini mwako jina nguruwe linapotajwa?

Bila shaka ni mambo yote ya kuchukiza kama vile uvundo, ulafi, uchafu na mambo mengine mengi ya kuchefua.

Hizi dhana hazipo akilini mwa Minneh Wanjiru Mburu ambaye amekuwa akifuga nguruwe kwa takribani miezi saba sasa.

Hakuwa na budi kuwatuliza majirani waliomwona kama tishio kwa mazingira yao na hewa safi waliyofurahia eneo hilo.

Hilo halikumvunja moyo maadamu mama huyu mwenye watoto wawili na ambaye amepania kukosoa kasumba zote potovu kuhusu nguruwe na kudhihirisha kwamba ufugaji wa nguruwe pia una upande wake wa kuvutia ikiwemo faida chungu nzima kwa mkulima.

“Nilipoanza, ilibidi nikabiliane na vikwazo kutoka kwa majirani zangu ambao hawakufurahi maadamu walihofia uvundo na uchafu unaohusishwa na nguruwe,” anasema Minneh.

Bi Minneh Wanjiru Mburu, mfugaji wa nguruwe Limuru. Picha/ Mary Wangari

Alianza kufuga nguruwe Januari 2019 na kulingana naye, hana majuto yoyote kufikia sasa.

“Mifugo wangu wa kwanza walikuwa nguruwe wawili waliokuwa na mimba. Nguruwe hao walikwisha zaa vivinimbi wengi wenye afya na kuongeza idadi yao. Vilevile, nimefanikiwa baada ya muda kuongeza nguruwe wengine zaidi wa kike na nguruwe mmoja wa kiume,” anasema.

Safari yake imekuwa taswira halisi ya ukakamavu na ustahimilivu na kuambatana na hulka yake ya ubunifu, ameanza kutumia mitandao ya kijamii kupitia ukurasa wa Facebook kwa jina Limuru Hog Wash, kutangaza bidhaa zake.

Mcheza kwao hutuzwa na hivyo ameanza kuona matunda ya kazi yake.

“Kwa sasa, sijaanza kuuza lakini idadi ya watu wanaowasiliana nasi na kufanya oda kupitia ukurasa wetu wa Facebook inatutia moyo sana na kutupa matumaini,” anasema.

Akilimali ilitaka kujua ni nini hasa kilichomchochea mkazi huyu wa eneo la Limuru kujihusisha na ufugaji wa nguruwe miongoni mwa aina zote za kilimo?

Kulingana naye, amewapenda nguruwe tangu utotoni mwake.

Jambo hili pamoja na haja inayoongezeka kila uchao ya nyama ya nguruwe ilimpa ari ya kujitosa katika ufugaji huo..

Licha ya hayo, safari yake haijakosa vikwazo na alikuwa na mengi ya kujifunza jinsi anavyosimulia.

Dhana moja potovu ambayo watu wengi wanashikilia kuhusu nguruwe ni kwamba ni walafi, wanakula sana na wanakula kila kitu.

Lakini jinsi anavyotufahamisha, nguruwe hula kiasi kidogo cha chakula wakilinganishwa na kuku na ng’ombe.

“Wanachohitaji nguruwe ni maji mengi, sio chakula kingi. Nguruwe wanahitaji maji kwa wingi kuliko chakula. Mwanzoni hili lilikuwa tatizo kwangu kwa kuwa maji tunayotumia eneo hili ni ya kununua,” anasema.

“Tatizo lingine lilikuwa kupata huduma ya afisa wa kutibu mifugo ambaye tungemtegemea. Hata hivyo, kwa sasa nina afisa wa kutibu mifugo ninayeweza kumtegemea anayewashughulikia mara kwa mara kila inapohitajika,” anaeleza.

Kwa wanaotamani kuanza kufuga nguruwe lakini wanahofia uvundo na uchafu, Minneh ana ushauri kutokana na tajriba yake binafsi.

“Jibu ni usafi. Weka chumba cha kuwafugia nguruwe wako kikiwa safi kila mara. Jambo lingine la kutilia maanani ni kile unachowalisha nguruwe wako. Kuna dhana kwamba nguruwe wanaweza kula kila kitu ikiwemo mabaki ya chakula na taka,”

“Hii ni kasumba potovu maadamu kuna aina mbalimbali ya vyakula mahsusi vya nguruwe vinavyosheheni viinimwili vyote wanavyohitaji. Lishe hiyo pia husaidia kuweka chumba kikiwa safi na kuzia uvundo,” anasema.

Kwa matokeo bora, ni muhimu kufahamu kwamba unapaswa kuwatunza kwa makini nguruwe wako ambao pengine itakushangaza, lakini ni wanyama watulivu jinsi anavyowaelezea kwa upendo.

Anafichua kwamba, ikilinganishwa na aina nyinginezo za kilimo, mtaji wa kuanza ufugaji wa nguruwe si ghali.

“Changamoto kuu ni ujenzi wa zizi la nguruwe na kuwapata nguruwe wa kike. Lishe ya nguruwe ni ya bei nafuu unayoweza kumudu kirahisi,” anasema akitufichulia kwamba alianza na mtaji wa Sh200,000 aliopata kutokana na akiba yake binafsi na usaidizi kutoka kwa famiia yake.

Minneh ambaye pia anashiriki kilimo cha bidhaa za chakula, anawarai watu wengine kujiunga na kilimo hiki akisema kwamba bado pana haja kubwa.

Kulingana naye, soko bado ni pana nab ado halijatoshelezwa hivyo hakuna haja ya kuhofia litajaa hivi karibuni.

“Ninawahimiza watu wengine zaidi kujitosa katika aina hii ya kilimo kwa sababu inazidi kutia fora na haja ya nguruwe haijatoshelezwa. Soko lingali pana mno hivyo hamna wasiwasi,” anasema.

“Hata hivyo, sawa na aina nyingine yoyote ya kilimo, hakikisha unafanya utafiti wa kina na ujihami na maarifa ya kutosha,” anatahadharisha, akiongeza kwamba wakulima wanapaswa pia kuhakikisha wana nafasi ya kutosha ya kujengea zizi la nguruwe.

 

[email protected]

You can share this post!

2022: Uhuru amuacha Ruto mataani

Aliyekuwa mkurugenzi wa KVDA akamatwa

adminleo