• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Madiwani ngome ya Ruto waunga mkono ‘Punguza Mizigo’

Madiwani ngome ya Ruto waunga mkono ‘Punguza Mizigo’

Na WAANDISHI WETU

MABUNGE ya kaunti za Kaskazini mwa Rift Valley yameapa kupitisha Mswada wa Punguza Mizigo unaopendekeza marekebisho ya katiba kutoka kwChama cha Thirdway Alliance, ambao tayari yameupokea.

Madiwani wa kaunti za Baringo, Uasin Gishu, Nandi, Pokot Magharibi na Elgeyo Marakwet, jana walisema Baraza la Mabunge ya Kaunti litaunga mkono mswada huo lakini wataangalia kama unafaa kufanyiwa kwanza marekebisho.

“Wakenya wameteseka kwa muda mrefu kwa sababu katiba imewalemea sana na inahitaji kurekebishwa. Kuna nafasi kadhaa za kisiasa kama za Maseneta na Wabunge Wawakilishi wa Kike Kaunti ambazo majukumu yao yanafanana na ya mamlaka mengine yaliyopo na zinafaa kuondolewa ili kupunguzia wananchi mzigo,” akasema Diwani wa Silale, kaunti ya Baringo, Bw Nelson Lotela.

Mswada huo tayari umepingwa na Chama cha ODM kinachoongozwa na Bw Raila Odinga, pamoja na Wiper kikiongozwa na Bw Kalonzo Musyoka.

Bw Odinga amekuwa akipendekeza katiba irekebishwe ili kuwe na mfumo wa uongozi utakaorudisha wadhifa wa Waziri Mkuu mwenye mamlaka makubwa kitaifa, lakini Naibu Rais William Ruto humpinga.

Diwani Maalum katika Kaunti ya Baringo, Bw Francis Kibai alisema kubuniwa kwa hazina ya fedha ya wadi kutawezesha wananchi kufurahia matunda ya ugatuzi.

Spika wa Bunge la Kaunti ya Uasin Gishu, Bw David Kiplagat alisema mabunge ya Rift Valley yatakutana hivi karibuni kutoa msimamo wa pamoja kuhusu mswada wa Punguza Mizigo.

“Tangu mwanzo, mswada huu ulionekana kuwa jambo jema. Nadhani ni mwelekeo unaofaa,” akasema Bw Kiplagat.

Hata hivyo alitilia shaka baadhi ya sehemu zake ambazo alisema zitahitaji marekebisho kwanza kama sehemu zinazopendekeza mishahara.

Alisema jukumu la kutahtmini mishahara ni la Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) kikatiba na tume hiyo ni huru.

Madiwani wa Kaunti ya Nandi wakiongozwa na Diwani wa Wadi ya Lessos, Bw Emmanuel Mengich na mwenzake wa Terik, Bw Osborne Komen pia waliunga mkono mswada huo ambao utapelekea idadi ya wabunge kupunguzwa, na wadhifa wawakilishi wa kike kaunti kuondolewa.

Diwani wa Kilibwoni, Bi Cynthia Muge na Mbunge Maalum, Bi Theresa Maiyo walisema Wakenya wanateseka kwa ajili ya kiwango kikubwa cha fedha kinachotumiwa kulipa watumishi wa umma, wabunge na viongozi wengine wa kisiasa ambao wengi wao hawachangii chochote kuleta maendeleo ya kiuchumi nchini.

“Baadhi ya wabunge na madiwani hawajawahi kutoa mchango wowote bungeni katika nchi hii na kazi yao ni kupata mishahara bila kufanya kazi yoyote,” akasema Bw Komen.

Kwa upande wake, Bw Mengich alisema: “Wakenya wanateseka kwa sababu kuna viongozi wasiofikiria na wasioweza kufanya maamuzi yao kwa njia huru. Wakati mwingi viongozi aina hii hushawishiwa katika misimamo wanayochukua kuhusu masuala yanayohusu kaunti na taifa kwa jumla. Katika Kaunti ya Nandi tunaunga mkono mswada wa Aukot ili kuboresha Kenya kwa manufaa yetu wote.”

Ripoti za Wycliff Kipsang’, Tom Matoke, Florah Koech, Evans Kipkura, Sammy Lutta na Oscar Kakai

You can share this post!

Maoni ya wananchi kuhusu kamari

Magoha akosoa vyuo vikuu kwa kupinga azma ya kuviunganisha

adminleo