Mwamba wachukua uongozi katika raga ya kitaifa
Na GEOFFREY ANENE
MABINGWA wa zamani Mwamba wamechukua uongozi wa raga ya kitaifa ya wachezaji saba kila upande kutoka kwa wanabenki wa KCB baada ya kutwaa taji la duru ya pili ya Kabeberi Sevens mnamo Jumapili mjini Meru.
Vijana wa kocha Kevin Wambua ambao walimaliza duru ya ufunguzi ya Kakamega Sevens katika nafasi ya tatu zaidi ya wiki moja iliyopita, wako juu ya jedwali kwa alama 39.
Washindi hawa wa mwaka 2007, 2008, 2010 na 2011 wamefungua mwanya wa alama mbili dhidi ya wafalme wa mwaka 2013 na 2014 KCB waliokamilisha ziara ya Meru katika nafasi ya nne.
Washindi wa mwaka 2015 Nakuru, ambao waliingia duru hiyo ya pili wakishikilia nafasi ya nne, wameruka juu nafasi moja baada ya kuimarisha alama zao kutoka 15 hadi 32 kwa kuambulia nishani ya shaba uwanjani Kinoru siku ya Jumapili.
Nakuru, ambayo itaandaa duru ya nne ya Prinsloo mnamo Agosti 17-18, iko sako kwa bako kwa alama 32 dhidi ya wafalme wa mwaka 2016 Homeboyz, ambao pia wanatetea taji baada ya kunyakua taji mwaka jana. Hata hivyo, Homeboyz wameshuka nafasi mbili hadi nambari nne.
Majirani wa Nakuru, Menengai Oilers ndio waliimarika zaidi baada ya duru ya pili. Oilers waliomaliza duru ya ufunguzi mjini Kakamega katika nafasi ya tisa kwa alama nane, sasa wanakamata nafasi ya tano kufuatia kampeni yao safi mjini Meru iliyoishia katika nafasi ya pili. Timu ya Oilers imevuna jumla ya alama 27.
Nafasi ya sita na saba
Nondies na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Masinde Muliro (MMUST) wamekwamilia katika nafasi ya sita na saba mtawalia.
Timu ya Nondies ilijiongezea alama 12 ilizokuwa nazo kutoka Kakamega Sevens na sasa inajivunia kukusanya jumla ya alama 24.
MMUST pia ilizoa alama 10 mjini Kakamega na idadi hiyo ya alama kutoka mjini Meru. Strathmore Leos inafuata katika nafasi ya nane kwa alama sawa na MMUST.
Leos, ambayo iliibuka bingwa wa Kenya mwaka 2009, ilisukumwa kutoka nambari tano hadi nane baada ya kurukwa na Oilers, Nondies na MMUST kwa sababu ya kukosa kufika robo-fainali kuu Jumapili.
Washindi wa mataji ya mwaka 1999, 2000, 2001 na 2004 Impala Saracens pia wamejipata wakiteremka kwenye jedwali la ligi hii ya duru sita baada ya kukosa kuingia mduara wa nane-bora wa Kabeberi Sevens.
Impala wametoka nafasi ya nane na kutulia katika nafasi ya tisa kwa alama 18. Wanafuatiwa na wa timu ya Mean Machine kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi, ambayo imesalia katika nafasi ya 10 kwa alama 12.
Northern Suburbs Cubs, ambayo ilipandishwa ngazi kushiriki mashindano ya daraja ya juu ya Kabeberi baada ya kushinda ya daraja ya pili mjini Kakamega, inapatikana katika nafasi ya 11 kwa alama 10.
Inafuatiwa na Egerton Wasps, Blak Blad, mabingwa wa zamani Kabras Sugar na Kenya Harlequin pamoja na Western Bulls, Catholic Monks, Kisii, Meru na Kisumu ambazo hazifikisha alama 10.