• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:38 AM
SHINA LA UHAI: Nasuri ya Uzazi yawanyima kina mama starehe

SHINA LA UHAI: Nasuri ya Uzazi yawanyima kina mama starehe

Na PAULINE ONGAJI

SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) linakadiria kwamba zaidi ya wanawake milioni mbili duniani wanakumbwa na ugonjwa wa Nasuri ya Uzazi (Obstestric Fistula).

Nasuri au Fistula huelezwa kwamba ni shimo au tundu baina ya uke na rektamu au kibofu cha mkojo, linalosababishwa na uchungu wa uzazi kwa muda mrefu (prolonged labour), suala linalomfanya mwanamke ashindwe kudhibiti mkojo, kinyesi au vyote.

Kwa Muthoni, 35, ni tatizo lililomkumba kwa miaka 13, hadi majuma manne yaliyopita, alipobahatika kuwa mmoja wa wanawake 115 waliofanyiwa upasuaji bila malipo katika hospitali kuu ya kitaifa ya Kenyatta, kupitia kampeni ya Vesical Vaginal Fistula (VVF): Medical Camp iliyoshirikisha hospitali hiyo na kampuni zingine tatu.

Tatizo lake lilianza mwaka wa 2006 baada ya kujifungua mtoto wake wa kwanza.

“Nilijifungua mtoto wangu nikiwa nyumbani kwa usaidizi wa mkunga,” aeleza Muthoni.

Anasema kwamba baadaye aligundua anashindwa kudhibiti kinyesi. “Ilinibidi kuwa na mazoea ya kwenda chooni kila nilipohisi haja,” asema.

Hata hivyo mambo yaligeuka na kuwa mabaya zaidi Agosti 23, 2017 alipokuwa akijifungua mwanawe wa pili.

“Nakumbuka nilikuwa hospitalini katika wadi ya kujifungua ambapo kama kawaida madaktari walikuwa wakija kufanya utaratibu wa kawaida kuchunguza ikiwa lango la uzazi lilikuwa limepanuka. Nikiwa hapa nilimsikia daktari akiwauliza wahudumu kwa nini walikuwa wameniacha niumwe kwa muda mrefu ilhali walikuwa wanajua kwamba nilikuwa na fistula,” anaeleza.

Anasema kwamba alishtuka sana lakini anakiri bado hakujua kiwango cha jeraha alilolokuwa nalo.

Hata hivyo alikumbana na hali halisi baada ya kujifungua na kuruhusiwa kwenda nyumbani. “Japo nilijifungua kupitia upasuaji, baadaye nilikumbwa na tatizo la kushindwa kudhibiti sio tu mkojo, bali pia kinyesi na hata hedhi wakati wa mwezi,” asema.

Tangu hapo maisha yake yalibadilika.

“Niliacha kabisa kuvaa chupi, na badala yake nikaanza kuziba kwa matambara ya nguo ili kudhibiti uchafu uliokuwa ukitoka, vile vile harufu mbaya,” asema.

Aidha, nililazimika kukagua vyakula nilivyokuwa nikila na kwa wakati upi.

“Singeweza kula vyakula vyepesi kwani hiyo ilikuwa mbinu yangu ya kuzuia kinyesi chepesi ambacho kingetoka upesi kikilinganishwa na kile kigumu ambacho angaa kilinipa onyo na muda wa kufika msalani,” aeleza.

Mbali na hayo alilazimika kupiga marufuku safari za mbali kama mbinu ya kuzuia aibu inayotokana na kujichafua katika maeneo ya umma.

“Hata safari fupi pengine kutoka nyumbani hadi katikati mwa jiji la Nairobi, zilihitaji mpango maalum. Kwa mfano lazima ningehakikisha kwamba nina nepi za watu wazima kwani singetembea nikiwa nimevalia matambara. Vilevile nililazimika kuhakikisha kwamba nala vyakula vigumu kupunguza mkojo na kukausha kinyesi,” asema.

Lakini tatizo kuu asema, lilikuwa unyanyapaa kutoka kwa jamaa wa karibu huku akilazimika pia kukatiza mahusiano ya kimapenzi. “Tangu Novemba 2016 niliposhika mimba ya mwanangu wa pili, sijawahi tena kuwa katika uhusiano wa kimapenzi,” aeleza.

Naye Bi Chebet, mkazi wa eneo la Bomet, asema tatizo lake lilianza mwaka wa 1993 baada ya kujifungua mtoto wake wa kwanza na wa kipekee. Kwake alishindwa kudhibiti mkojo, suala lililomlazimu kukaa nyumbani kwake kila wakati.

“Nilijaribu kwenda katika hospitali kadha bila usaidizi, na hivyo ikanibidi nizoee hali yangu. Kwa mfano, singeweza kuenda safari ya mbali sababu ya nilihitaji kubadilisha matambara yangu, kuyasafisha na kuyaanika kila mara. Aidha singemudu bei ya nepi za watu wazima,” asema.

Tatizo hili liliathiri pia ndoa yake na hivyo miaka mitatu iliyopita alilazimika kurejea nyumbani kwao ili kutafuta matibabu.

Wawili hawa ni miongoni mwa wanawake 115 waliobahatika kunufaika kutokana na upasuaji bila malipo katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta kati ya Juni 27 hadi Julai 12 mwaka huu.

Wawili hawa wanawakilisha idadi inayozidi kuongezeka ya wanawake wanaokumbwa na hali hii humu nchini.

Hapa nchini, kila mwaka kati ya visa 1,000 na 3,000 vipya hugunduliwa huku kati ya wanawake watatu na wanne kati ya 1,000 wanaojifungua wakikumbwa na hali hii.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa mwaka wa 2011 na Campaign To End Fistula, kuna kati ya visa 1,000 na 3,000 vipya vya fistula kila mwaka nchini Kenya, huku asilimia 7.5 pekee ya waathiriwa wakiwa na uwezo wa kufikia huduma ya kimatibabu.

Nchini Kenya, ugonjwa huu husababisha angalao 6% ya vifo vya akina mama wajawazito huku tatizo linalozidi kuwakumba wengi likiwa ni gharama kubwa ya matibabu.

Katika hospitali za kibinafsi nchini, gharama ya matibabu ni kati ya Sh250, 000 na Sh450, 000 huku katika hospitali za umma gharama ikiwa kati ya Sh50,000 na Sh90,000.

Ripoti iliyowasilishwa na Hazina ya Shirika la Umoja wa kimataifa kuhusu idadi ya watu- UNFPA ya mwaka wa 2004, ilionyesha idadi ya wagonjwa wanaokumbwa na hali hii na ambao hawajapata matibabu imefikia 300,000.

Tatizo hili linaonekana kukumba zaidi mataifa yanayostawi, ikilinganishwa na nchi zilizoendelea. Kwa mfano, takwimu zinaonesha kwamba kila dakika mwanamke mmoja hufariki kutokana na matatizo ya kujifungua duniani, huku asilimia 95 wakiwa kutoka barani Afrika na Asia.

Haya yakijiri, kuna afueni kuu katika mataifa yaliyostawi.

Hospitali kufungwa

Kwa mfano, hospitali ya mwisho kutibu fistula nchini Amerika ilifungwa mwaka wa 1895.

Dkt Khisa Wakasiaka, mwanajinakolojia na daktari wa upasuaji anayehusika na masuala ya fistula katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) anasema tatizo hili limekithiri sana katika maeneo ya mashambani ambapo huduma kwa akina mama wajawazito haipatikani kwa urahisi au ni duni.

Anasema kwamba japo tatizo la kuziba kwa njia ya uzazi wakati wa kujifungua hutokea katika sehemu zote duniani, tunapaswa kuwa na uwezo wa kukabiliana nalo.

“Hatuwezi kuzuia wanawake kushika mimba, lakini pia wanapaswa kujifungua bila kusababishiwa ulemavu,” asema Dkt Wakasiaka.

Kulingana na Dkt Dan Okoro, mtaalamu wa masuala ya afya ya uzazi, sharti akina mama wahakikishiwe huduma ya ubora wa hali ya juu wakati wa ujauzito na wanapojifungua. “Matatizo mengi hutokea kutokana na huduma duni wanapojifungua. Japo hakuna hakikisho la kuzuia majeraha wakati huu, hayapaswi kubadilika na kuwa ulemavu,” aeleza.

Kulingana na Dkt Khisa, tiba ya nasuri ya uzazi haihusishi tu upasuaji wa kurekebisha ulemavu uliosababishwa na kujifungua, bali pia kukabiliana na majeraha ya kisaikolojia.

“Wagonjwa wengi hupitia aibu na unyanyapaa unaosababisha kudorora kwa viwango vya kujithamini, kumaanisha kwamba endapo tunataka kuwarejeshea thamani yao, basi lazima pia tiba ya kiakili ihusishwe,” aeleza.

You can share this post!

VIDUBWASHA: Utaweza kujipima macho ukiwa nyumbani (The...

Wakulima wataka ripoti ya jopokazi la sukari iwekwe wazi

adminleo