Masoud Juma asajiliwa sasa nchini Algeria
Na CHRIS ADUNGO
FOWADI wa Harambee Stars, Masoud Juma amepata hifadhi mpya kambini mwa Jeunesse Sportive de Kabylie nchini Algeria.
Nyota huyu ambaye hajakuwa na klabu, amerasimisha uhamisho wake kwa mkataba wa miaka mitatu.
Klabu ya mwisho kumsajili ni Al-Nasr Benghazi ya Libya ambayo iliagana naye bila ya hata kumwajibisha katika mchuano wowote.
Kiini cha kuvunjika kwa mkataba kati ya Masoud na waajiri wake hao ni msukosuko wa kisiasa uliowahi kushuhudiwa katika taifa la Libya.
Licha ya kusalia nje ya ulingo wa soka bila ya kusakatia klabu yoyote, Masoud alikuwa sehemu ya kikosi cha Harambee Stars kilichotegemewa na kocha Sebestien Migne katika fainali za Kombe la Afrika (AFCON) zilizokamilika majuzi nchini Misri.
Hadi alipoingia katika sajili rasmi ya Kariobangi Sharks waliompa jukwaa la kung’aa zaidi, Masoud alikuwa amewachezea pia Bandari FC na SoNy Sugar waliotawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) kwa mara ya mwisho mnamo 2006.
Ushawishi wa Masoud kambini mwa Sharks mnamo 2017 ulimfungulia milango ya kusajiliwa na kikosi cha Cape Town City nchini Afrika Kusini baada ya kutawazwa Mfungaji Bora wa KPL msimu huo.
Kuimarisha safu ya uvamizi
Hata hivyo, alihudumu katika kikosi cha Cape Town City kwa kipindi kifupi kabla ya maarifa yake kuwaniwa na klabu ya Dibba Fujairah katika Nchi za Milki za Kiarabu (UAE) mnamo Septemba 22, 2018.
“Tunataraji kwamba ujio wa Masoud utafufua zaidi makali ya safu yetu ya uvamizi kadri tunavyojiandaa kunyanyua ubingwa wa Ligi Kuu ya Algeria msimu huu,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa jana na vinara wa kikosi cha JS Kabylie.
Mnamo Juni 2017, Masud aliwahi kufanyiwa majaribio na kikosi cha AIK Jonkopings Sodra kutoka Uswidi kisha kuyoyomea Bidvest Wits ya Afrika Kusini ambayo pia ilimfanyia majaribio ya wiki tatu mnamo Julai mwaka huo. Japo yalikuwa matamanio ya Wits kumsajili Masoud, nyota huyu alihiari kutua kambini mwa Cape Town City mnamo Januari 2018. Mchuano wa mwisho kwa Masoud kuwajibikia timu ya taifa ya Harambee Stars ni ule uliowakutanisha na Sierra Leone katika safari yao ya kufuzu kwa fainali za AFCON 2019.