Michezo

GUMZO LA SPOTI: Zidane amtaka Pogba kikosini

July 31st, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

MADRID, Uhispania

KLABU ya Madrid imesisitiza kwamba lazima imchukue kiungo mahiri Paul Pogba anayechezea Manchester United.

Kocha Zinedine Zidane amesema anamtaka Mfaransa huyo kwa lengo la kuimarisha kikosi chake pale ugani Santiago Bernabeu.

Hata hivyo, imedaiwa lazima Rais Florentino Perez ashawishiwe sana baada ya Madrid kutumia kiasi kikubwa cha pesa muhula huu wa kiangazi.

Habari kutoka klabuni hapo zinasema kwamba Madrid imetumia zaidi ya Sh35 bilioni kununuwa wachezaji wapya kwa ajili ya msimu ujao.

Pogba kupitia kwa ajenti wake, Mino Riaola amesisitiza kuwa wakati wa kuondoka Old Trafford umefika hata baada ya juhudi za mara kwa mara za kocha Ole Gunnar Solskjaer kumsihi abakie.

Awali, Perez aliwaambia waandishi kwamba wameshindwa kumpata Pogba kwa sababu Manchester hawajaamua kumuuza, lakini kuna madai kwamba kuna maelewano yanayokaribia kumalizika.

Asensio aumia

Madrid inapigania nyota huyo baada ya Marco Asensio kuumia vibaya ambapo anatarajiwa kuwa nje kwa muda mrefu; na Zidane anaamini mtu wa kujaza nafasi hiyo ni Pogba kutokana na ubora wake katika safu ya kiungo na pia kama mshambuliaji.

Zidane anataka kuimarisha safu ya ushambuliaji hata baada ya majuzi kumpata Eden Hazard kutoka Chelsea.

Katika mipango yake, Madrid wanatarajiwa kupokea Sh na kumuachilia James Rodriguez ambaye anatakiwa na majirani zao, Atletico Madrid.

Wakati huo huo, mshambuliaji matata Gareth Bale wa Real Madrid anakaribia kutimkia China kujiunga na mojawapo wa klabu maarufu nchini humo.

Bale aliyefunga mabao 31 katika mechi 77 akiwa na timu ya taifa ya Wales ameelezwa kuwa na mpango wa kujiunga na klabu ya Jiangsu Suning kwa mkataba wa miaka mitatu.

Tayari kocha Zidane amesikika akisema hatamzuia nyota huyo kuondoka kwa vile hayumo katika mipango yake ya baadaye.