• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
UFUGAJI: Tunza ng’ombe wa maziwa jinsi unavyoweza kutunza mtoto mchanga

UFUGAJI: Tunza ng’ombe wa maziwa jinsi unavyoweza kutunza mtoto mchanga

Na MWANGI MUIRURI

LISHE bora, kutobahatisha na magonjwa na usafi wa kimazingira ndio viungo muhimu katika kumtunza ng’ombe wa gredi ili naye shukrani yake iwe kukupa maziwa bila kipimo.

Bw Lawrence Munyua ambaye kwa miaka 37 sasa amekuwa katika sekta hii ya kuuza maziwa kutoka mradi wake wa uwekezaji kwa ng’ombe wa maziwa anasema kuwa ng’ombe mmoja wa maziwa ni lazima awekwe katika mpango maalumu wa kumpa kilo 15 za chakula kwa siku.

“Kilo hizo ni tano za nyasi kavu, saba za majani yaliyo na unyevu wa wastani, mbili za chakula cha maziwa na moja ya chakula za kuongeza maadini,” anasema Bw Munyua.

Anasema kuwa mfumo huo wa lishe unafaa kugawanywa kwa awamu mbili, asubuhi na jioni.

“Aidha, ni lazima ng’ombe huyo ahakikishiwe kiini cha maji na kwa wakati wowote ule asikose maji hayo,” anasema.

Anasema kuwa chakula hicho lazima kiwe na mchanganyiko wa 2:1:1 wa protini, chakula cha joto na nguvu na vitamini.

Anasema kuwa magonjwa hatari ya ng’ombe husababishwa na mazingira machafu, uokotaji wa chakula takataka na kuwapa mifugo hao pamoja na wadudu kama kupe, minyoo na hata kunguni.

“Ni vizuri uweke daktari wako wa matibabu ya mifugo ambaye kwa wiki atatembelea shamba lako na kukukagulia mifugo hao. Ni lazima utilie mkazo afya ya ng’ombe wako kwa kuwa gharama ya hasara iko juu sana kuliko ile ya kimatibabu,” anasema.

Kwa mfano, Bw Munyua anasema kuwa ikiwa ng’ombe wako ataugua ugonjwa ambao utakugharimu Sh2,000 kuutibu, lakini uzubae na hatimaye akufe, utapoteza takriban Sh500,000 hii ikiwa ni kadirio la pato la maziwa, thamani ya ng’ombe huyo na ndama ambao angekuzalia.

“Usicheze kamari na ng’ombe wako, mtunze kama mtoto mchanga ukijua waziwazi kuwa ikiwa utampoteza mwana kupitia ulegevu wa kumakinika kimatibabu, utakuwa unajipa kazi nzito,” anasema.

You can share this post!

Mahakama yamkausha Baba Yao

Je, wanafunzi wanafaa kuadhibishwa ama kwa kuzabwa kofi au...

adminleo