Makala

AKILIJIBU: Kuku wameanza ghafla kutaga mayai madogo, sababu ni gani?

August 1st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

SWALI: Jina langu ni JOSEPHAT MUSERA kutoka Chavakali, Vihiga. Nimekuwa mfugaji wa kuku kwa muda mrefu, lakini hivi karibuni nimeshangazwa na jinsi ambavyo wameanza kutaga mayai madogo. Je, ni nini kiini cha mabadiliko haya?

JIBU: Yapo mambo mengi yanayoweza kuchangia hali hii. Mojawapo ni umri wa kuku. Kuku wengi wanapoanza kutaga, huwa wanataga mayai madogo madogo lakini kadri siku zinavyozidi kwenda huongezeka ukubwa hivyo kama wana umri wa wiki 32 na kuendelea, hawawezi kuwa na tatizo hilo isipokuwa sababu zingine zinaweza kuchangia.

Vinasaba vya kuku, lishe, ugonjwa na msongo ni sababu nyingine.

Kuna kuku wengine vinasaba vyao huwafanya kutaga mayai madogo tu na hivyo hata uwafanyeje, hawawezi kutaga mayai makubwa. Hivyo, hiyo ndio itakuwa hali yao ya kila siku.

Msongo unaweza kusababishwa na joto kali ndani ya banda, ukosefu wa maji, ukosefu wa hewa ya kutosha pamoja kuzidi kwa mwanga ndani ya banda. Vilevile wakati mwingine, msongo huweza kusababishwa na wanyama wakali kuingia bandani.

Mara nyingi kuku wenye wiki zaidi ya 32 wakikosa protini na chumvi ya kutosha husababisha kutaga mayai madogo. Pia inashauriwa sana kuhakikisha unabadili chakula mapema kutoka hatua moja ya ukuaji kwani nayo inaonekana kuwa ina mchango katika utagaji wa mayai madogo. Pia hakikisha kuku wako wanapata chakula wanachostahili pamoja na maji kwa siku. Magonjwa kama vile ya minyoo na ‘egg dropping syndrome’ yanaweza kusababisha kushuka kwa utagaji na wakati mwingine kutaga mayai madogo madogo. Hakikisha kuku wako wanapata dawa ya minyoo kila baada ya miezi mitatu.

SWALI: Ninaitwa JUNE NATALIE kutoka Voi. Mimi ni mkulima maarufu wa nanasi japo sijasoma sana. Natatizika kuwashawishi baadhi ya watu kununua mazao yangu hasa wanaponiuliza faida za nanasi mwilini. Niambieni tafadhali.

JIBU: Nanasi ni mojawapo ya matunda yaliyo na uwezo wa kuboresha afya yako. Cha msingi zaidi, nanasi hutumika kama dawa ya kuulinda mwili mwako. Nanasi ina kimeng’enya kinachoitwa bromelain. Husaidia kutibu vitu mbalimbali mwilini lakini ni madhubuti kwa kupunguza uvimbe wa ngozi kutokana na maambukizi au vidonda. Bromelain ni madhubuti pia katika kupunguza mauvimu ya viungo au uvimbe sugu. Kimeng’enyo hiki pia kina kemikali zinazosaidia kuangamiza seli za uvimbe mwilini.

Nanasi huwa na vitamin C kwa wingi pamoja na vitamin A, B1, B6, nyuzinyuzi (fiber), calcium, phosphorous na potassium ambayo huimarisha mifupa kutokana na madini ya manganese.

Kimeng’enya cha bromelain pia hutumika kuvunja (breakdown) molekuli za protini, ndio maana juisi ya nanasi hutumika kwenye marinade kulainisha nyama.