• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
Mhudumu katika baa aliyekuwa na ndoto ya kuwa wakili

Mhudumu katika baa aliyekuwa na ndoto ya kuwa wakili

Na MWANGI MUIRURI

MWAKA 2010 Ann Njeri akiwa mwingi wa matumaini maishani alifanya mtihani wa kufuzu elimu ya sekondari (KCSE) na akatulia nyumbani akisubiri matokeo.

Hata hivyo, anasema alipata mimba.

“Maisha yangu yalibadilika kutoka kwa yule aliyekuwa akisubiri matokeo ya mtihani ili ajiunge na elimu ya juu. Nikawa nangojea kuitwa mama,” anasema Njeri.

Matokeo yakitoka alikuwa amepata alama ya B-.

Wakati huo alikuwa kwa aliyempa mimba.

Anasema kuwa alikuwa amekubali ‘matokeo’ ambapo alitazamia kuwa mke mwema badala ya mwanafunzi mwema wa taaluma ya uwakili ambayo alikuwa akienzi katika maisha yake.

Miezi tisa baadaye, alijifungua mtoto wa kike na anasema kijana mwenye hiyo mbegu tayari alikuwa ameingiza kila aina ya dharau katika uhusiano huo na ambapo “hata wazazi wake walinionyesha waziwazi kuwa hawakunitaka.”

Anasema kuwa akiwa katika hospitali ya Maragua ambapo alijifungulia mtoto huyo hakuna mmoja wa familia hiyo aliyemtembelea wala kwenda kumchukua “tupeleke mtoto wao nyumbani.”

Anasema hata wakati aliwauliza mtoto apewe jina gani – kwa kuwa katika tamaduni za jamii ya Agikuyu mtoto wa kwanza hupewa jina la ama baba au mama wa mume – walisema hawakuwa na pendekezo lolote.

“Ni hapo ndipo nilijua kuwa nilikuwa nimepewa ‘talaka’. Huyu ni mimi na huyu ni mtoto wangu na sina pa kwenda kwa kuwa babake na watu wao walikuwa wamenikataa… Nilipiga moyo konde na nikajiambia kuwa Mungu aliyenijalia ujauzito huo, akanipa afueni ya kuzaa salama salmini, alikuwa bado katika kiti chake cha enzi na kamwe singejidunisha kiasi cha kukumbwa na msongo wa mawazo,” anasema.

Anasema aliamua kutorejea kwao nyumbani kwa kuwa wazazi wake nao walikuwa wamekereka si haba kutokana na tukio hilo la kupata mimba.

“Alitoka katika hospitali na akamwendea rafiki wake aliyekuwa akifanya kazi ya kuuza kwa baa. Nilikaa naye na urafiki wa kweli nikauona kwa macho. Rafiki huyo wangu alikuwa akinishughulikia kwa kila hitaji kwa miezi sita mfululizo na kamwe hakunionyesha kuwa nilikuwa mzigo kwake,” anasema.

Anaeleza: “Nilikula, nikalala, nikanywa, nikaoga, nikapata nguo za mtoto na pesa za kujisimamia kutoka kwa mwanadada huyo rafiki yangu.”

Anamuombea mwanadada huyo awe wa kubarikiwa katika kila kona ya maisha yake.

“Baada ya miezi sita, nilimweleza mwanadada huyu rafiki yangu kuwa nilitamani sana nifanye kazi ili nianze kujisimamia. Alinishauri ningoje mtoto wangu afikishe angalau umri wa mwaka mmoja ili iwe rahisi hata kumwacha katika shule za kuwalea watoto nikichapa kazi. Alinipa moyo kuwa nikome kujiona kama mzigo kwa kuwa hakuwa amechoka kunisaidia. Nililia machozi ya shukrani,” anasema.

Kujitolea kwa rafiki

Mwaka mmoja uliisha na huyo rafiki yake akamuulizia kazi katika baa aliyokuwa akiifanyia kazi na ndipo alikumbana na kujitolea na kujituma kwa rafiki yake kumfadhili kimaisha.

Imagine (Hebu fikiri) alikuwa akilipwa mshahara wa Sh6,000 na akiwa mama kwa watoto wake wawili ambao walikuwa chini ya malezi ya mamake mashambani, alinichukua pamoja na mtoto wangu na akawa akinitengea bajeti ya usaidizi. Niseme nini kwa ukarimu wa kiwango hicho?” anahoji.

Alipoanza kupata mshahara wake, aligundua afueni yake kuu ilikuwa kujipanga kibajeti na atumie ubunifu wa kupata pesa za ziada.

“Gharama ya kulipa nyumba kwa sasa ni Sh3,500. Kuna yaya ambaye mimi humlipa Sh3,000. Kuna gharama ya chakula, maji na stima ilhali mshahara wangu ni Sh6,000 na ambao huwa unapunguzwa na hesabu za kazini ambapo ama nimepoteza bili ya mteja au nimevunja au hata nimetumia soda au kinywaji kingine katika baa,” anasema.

Anasema katika hali hiyo ngumu, “bado ninajiwekea akiba na kwa miaka minane sasa ambayo nimekuwa katika hii kazi ya kuuza kwa baa, nimefikisha Sh80,000 kama akiba.”

Anasema lengo lake ni kuwekeza katika baa yake, lengo ambalo anasema litatimia kabla ya mwaka 2022.

“Maisha huwa ni magumu ndio, lakini uamuzi ni wako: Ama upambane kujiweka katika mkondo wa kimaisha au usalimu amri uondoke chini ya majanga ya kusombwa na mawazo au umaskini. Na tukumbuke kufaana kama binadamu. Ikiwa sikusaidiwa na rafiki yangu ambaye utu ndio ulimwongoza, singeafikia nilipo kwa sasa,” anashauri.

You can share this post!

AKILIJIBU: Kuku wameanza ghafla kutaga mayai madogo, sababu...

Magoha aitaka Knec kuweka wazi mada zitakazotahiniwa kwenye...

adminleo