• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:21 PM
KIU YA UFANISI: Mshonaji viatu aliye na maono ya Ajenda Nne Kuu za Serikali

KIU YA UFANISI: Mshonaji viatu aliye na maono ya Ajenda Nne Kuu za Serikali

Na MARY WANGARI

KIWANGO chake cha chini cha elimu katu hakijawahi kumzuia kulala unono na kuota ndoto za mambo makubwa kama vile kuwa mshiriki wa Rais Uhuru Kenyatta katika kutimiza Ajenda Nne Kuu za Maendeleo kuhusu viwanda.

Peter Mwangi Wathuta, 45, ambaye ni mkazi wa Nyahururu, amejipatia umaarufu na kuwavutia wengi kutokana na ustadi wake wa kipekee katika tasnia ambayo kwa kawaida hudunishwa na watu wengi.

Kwa sasa Mwangi anajivunia kuwa mkufunzi, mwajiri na mbunifu katika sekta ya utengenezaji viatu na hadithu yake hakika ni ya kutia moyo.

Alisomea katika Shule ya Msingi ya Ngeresha, Laikipia ambapo alifika darasa la nane na hangeweza kuendeleza elimu yake.

Hata hivyo, hali hiyo haikumvunja moyo na hapo ndipo alipoamua kutia makali kipaji chake kwa kujipa mafunzo hatua iliyomwongeza maarifa na ubunifu hata zaidi.

“Nilianza kujifunza kazi ya kushona viatu mnamo 1991 katika duka la mzee mmoja mjini Nyahururu. Niliachana nayo kwa muda lakini nikairejelea mwaka wa 2014. Kwa sababu ni kipaji changu niliweza kupata ujuzi zaidi na kuvumbua mitindo mbalimbali ya ushonaji wa viatu,” anasema.

Kwa sasa, Mwangi anaendesha karakana ya kushonea viatu katika eneo la Nyayo Jua Kali mjini Nyahururu ambayo pia hutumika kama afisi yake. Aidha, anamiliki duka la kuuzia viatu mjini humo linalofahamika kama Laikipia Nyati, jina ambalo tulipenda kujua asili yake.

“Niligundua kwamba kaunti ya Laikipia ni mojawapo wa vivutio vya watalii kutokana na wanyamapori na hapo ndipo nilipata hilo jina,” alitufahamisha huku akitabasamu.

Fundi huyu wa viatu ambaye anatujulisha kwamba hii ndiyo kazi pekee anayoitegemea kumpa riziki, anatudokezea kwamba yeye hutengeneza viatu aina ya boots zinazosheheni lakabu ya Laikipia Nyati.

Wateja anaolenga ni pamoja na maafisa wa usalama, walinzi, wahudumu wa bodaboda na wananchi wa kawaida kwa jumla.

Mwangi ambaye bila shaka ana jicho pevu la kugundua fursa inapoibuka, anatufahamisha kwamba sekta ya ulinzi ina soko pana ambalo halijashughulikiwa ipasavyo.

“Kuwepo kwa mashirika ya utowaji huduma za usalama yanayoongezeka kila uchao ikiwemo maafisa wa utekelezaji sheria katika kaunti ni soko mojawapo ambalo hatuwezi kupuuza,” anasema.

Raslimali anazotumia kutengenezea viatu zinajumuisha ngozi halisi, godoro na turubai miongoni mwa vifaa vingine anavyonunua jijini Nairobi.

Kisha yeye huzisafirisha kwenye karakana yake ya viatu mjini Nakuru ambapo huanza mchakato wa kutengeneza viatu aina ya boots zenye kiwango cha juu cha ubora kauli inayothibitishwa na bei ya viatu vyake.

“Kwa siku ninaweza kutengeneza kama jozi sita za viatu ambapo kila jozi ninauza Sh2500,” anatueleza akitudokezea kwamba anaweza kupata takriban oda 10 katika mwezi mzuri.

“Katika msimu mbaya ninapata faida ya takriban Sh15,000 lakini katika msimu mzuri kiasi hiki kinaongezeka maradufu,” anatueleza.

Changamoto

Hata hivyo, sawasawa na biashara nyingine yoyote inayoinukia, Mwangi anatufahamisha kwamba safari yake haijakosa pandashuka.

“Kupata vifaa vya kutengenezea viatu ilikuwa changamoto kuu kwangu. Ilibidi hata nifanye vibarua mbalimbali ili niweze kununua hata cherehani kwa kuwa niliyokuwa nikitumia ilikuwa ya kukodisha,” anasema.

Matatizo mengine ambayo ni changamoto kuu anazokumbana nazo ni pamoja na ukosefu wa hela na soko jinsi anavyotufahamisha.

“Ukosefu wa mashine za kisasa za kutumia kukata na kuunda vipande vya ngozi na vifaa vingine vya kutengenezea viatu pia hufanya kazi yake kuwa kibarua kigumu maadamu yeye hulazimika kutumia mikono yake,” anatujulisha.

Hata hivyo, changamoto hizo hazijamzuia kusonga mbele na kuwa kielelezo kwa watu ambao hawakubahatika kupata elimu pamoja na vijana wanaohangaika kusaka kazi.

“Ushauri wangu kwa watu wasio na elimu kama mimi ni kwamba kuna mambo mengi unayoweza kufanya ili kukusaidia kujikimu maishani,” anasema. Aidha ana ndoto na maono makubwa ya kupanua biashara yake katika siku zijazo na kuweza kuchangia katika ajenda ya maendeleo nchini kwa kubuni nafasi za kazi kwa watu wengine.

“Ombi langu kuu ni lau ningeweza kupata msaada wa kupata mashine za kisasa. Hii itaniwezesha kutoa mafunzo na kuwaajiri watu wengi katika juhudi za kutimiza maono ya Rais wetu ya Ajenda Nne Kuu za Maendeleo kuhusu sekta ya viwanda,” anatueleza.

You can share this post!

Wakazi wa Mbagathi kupata shule ya upili mwaka 2020

KIU YA UFANISI: Polisi afugaye ng’ombe kwa ajili ya...

adminleo