• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 6:55 AM
KIU YA UFANISI: Polisi afugaye ng’ombe kwa ajili ya kuwauza

KIU YA UFANISI: Polisi afugaye ng’ombe kwa ajili ya kuwauza

Na PETER CHANGTOEK

PETER Mungai ni afisa wa polisi ambaye amewahi kuhudumu katika kitengo cha GSU katika maeneo kama vile Mandera na Tana River.

Pia, amewahi kuhudumu katika kikosi cha kumsindikiza rais (Presidential Escort). Kwa wakati huu, yeye huhudumu katika maskani ya rais mstaafu, Mwai Kibaki, katika eneo la Muthaiga, Nairobi.

Hata hivyo, licha ya jukumu hilo alilotwikwa na serikali, amekuwa maarufu mno kutokana na shughuli adhimu ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa.

Azma yake kuu ni kuwafuga ng’ombe wa maziwa na kuwauzia wateja walioko nchini na nje ya nchi.

Mungai aliajiriwa katika kitengo cha polisi mnamo mwaka 2007, na baada ya kuipata ajira hiyo, akaamua kuomba mkopo wa Sh400,000 ili kukianzisha kilimo hicho. Anasema alitumia baadhi ya fedha hizo kuwanunua ng’ombe wanne, alioanza nao.

“Nilichukua mkopo wa Sh400,000. Nilikuwa na bahati kwa sababu kulikuwa na shamba la babangu, ambaye alikuwa mwanajeshi,” afichua mkulima huyu, ambaye huendesha ufugaji katika kitongoji cha Gathigi, Kiambu.

Amelipa shamba hilo jina ‘Munene Farm’, ambalo ni jina halisi la babake.

Japo ndani ya shamba hilo mna wanyama wengine wa kufugwa kama vile kondoo na ndege kadha wa kadha, anasisitiza kuwa hao si wa kuuzwa, ila ng’ombe tu ndio anaowafuga kwa minajili ya kuwauza.

Kwa jumla, ana wafanyakazi saba, ambao humsaidia katika shughuli hiyo wakati yupo kazini.

“Wao hufanya kazi kwa zamu. Kabla sijamwajiri mfanyakazi mgeni shambani, yeye hupewa mafunzo. Wao hujipanga jinsi ya kufanya kazi- kuna wale ambao huwakagua ng’ombe usiku na kuwalisha,” asema, akiongeza kuwa ni jambo muhimu pia kuwatunza wafanyakazi vyema ili waridhike na kufanya kazi bora shambani.

Mkulima huyo anasema kuwa kwa wakati huu ana jumla ya ng’ombe 80, na zaidi ya asilimia 90 ya ng’ombe hao ni wa kike, na huwafuga idadi kubwa ya ng’ombe aina ya Friesian.

Mungai anafichua kuwa kwa siku moja, yeye hupata maziwa kati ya lita 300 na 350, na huyauza kwa kampuni ya maziwa ya Fresher Dairies.

Amewapa ng’ombe wake majina ya binadamu. Mja anapozuru vibanda vyao, hatakosa kuyaona majina kama vile Daisy, Rose, n.k, miongoni mwa ng’ombe wa kike; majina yaliyoandikwa kwa vijidude vya plastiki na kubandikwa masikioni pa mifugo hiyo.

“Tunayo rekodi ya kila ng’ombe. Wakati mkulima anaponunua ng’ombe, kwa mfano Daisy, ninabaki na namba yake ya simu ili chochote kikifanyika, nitajua kwa daktari wa mifugo ni matibabu yepi anafaa kupewa,” adokeza.

Anaongeza kuwa ni muhimu kuwapa ng’ombe majina mazuri.

“Wakati mwingine ni muhimu utathmini majina unayowapa wanyama wako, kwa sababu wanaweza kuwa na mienendo inayoambatana na majina hayo. Kwa mfano unaweza kumwita “Ufisadi” na utashangaa akianza kuwanyang’anya wengine lishe zao na kula,” asema na kutufanya tuangue kicheko.

Mungai hushughulika mno na ufugaji wa ng’ombe aina ya Freshian na Holsteins. Yeye humwuza ndama wa miezi minne hadi sita kwa bei ya Sh50,000-Sh60,000. Mwenye umri wa miezi sita hadi miezi kumi na miwili huuzwa kwa bei ya Sh70,000-Sh80,000, ilhali yule ambaye amewahi kuzaa mara moja huuzwa kwa Sh165,000-Sh170,000.

“Nimeweka mifereji na hutamwona mfanyakazi yeyote akitembea na ndoo ya maji ya kuwapa, ni kufungulia tu maji kwa mfereji,” aongeza mkulima huyo.

Anunua ploti

Kutokana na kilimo hicho, Mungai ameweza kuzinunua ploti sita na kujenga nyumba za kukodisha.

“Kupitia kwa biashara hii, nimenunua ploti sita. Nina ploti nne kule Kamulu, na mbili ambazo ninajenga kule Mwihoko, Githurai,” asema, akiongeza kuwa hupata Sh15,000 kwa kila nyumba kwa baadhi ya ploti zake.

Mkulima huyo, ambaye hupata wateja maeneo mathalani Kericho, Nandi, Nakuru, Narok, Eldoret, na kutoka nchini Tanzania na Uganda, anasema kuwa kujiajiri ni msingi wa fanaka kwa kila mja.

Ili kuhakikisha kuwa ng’ombe wake hawakabiliwi kwa urahisi na maradhi, ana daktari wa mifugo ambaye huishi Githunguri, ambaye huzuru shambani kila siku.

Mungai hushughulika mno na ufugaji wa ng’ombe aina ya Freshian na Holsteins. Yeye humwuza ndama wa miezi minne hadi sita kwa bei ya Sh50,000-Sh60,000. Mwenye umri wa miezi sita hadi miezi kumi na miwili huuzwa kwa bei ya Sh70,000-Sh80,000, ilhali yule ambaye amewahi kuzaa mara moja huuzwa kwa Sh165,000-Sh170,000.

Aidha, ng’ombe ambaye amewahi kuzaa mara mbili na huyazalisha maziwa lita 30, huuzwa Sh170,000-Sh180,000. “Lakini sisi hupunguza bei kulingana na idadi ya ng’ombe ambao mkulima hununua,” asema Mungai.

You can share this post!

KIU YA UFANISI: Mshonaji viatu aliye na maono ya Ajenda Nne...

Serikali yawatuma Israel wanafunzi 96 kufundishwa ukulima...

adminleo