Makala

ULIMBWENDE: Manufaa ya mafuta ya nazi

August 2nd, 2019 1 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

MAFUTA ya nazi ni mazuri kama yatatumika ipasavyo. Yana uwezo wa kukufanya uonekane mrembo mwenye ngozi ya kuvutia.

Miongoni mwa faida za kutumia mafuta ya nazi ni kama zifuatazo:

Kulainisha ngozi. Mafuta ya nazi yanasaidia kwa kiasi kikubwa sana kulainisha ngozi na kuipa afya nzuri.

Kuondoa magaga na mitembo kwenye nyayo za miguu na kuzuia mipasuko ya nyayo, kukauka kwa ngozi ya mikono.

Kuondoa ngozi iliyoharibika ‘Dead skin’

Mafuta ya nazi husaidia kuondoa ngozi iliyoharibika katika mwili wako, chukua mafuta ya nazi, sukari na chumvi changanya ili upate mchanganyiko mmoja kisha paka mwili mzima.

Fanya masaji kwa mchanganyiko huo na ukae nao kwa muda kisha oga vizuri kwa maji safi ukitumia sabuni. Utaona mabadiliko katika ngozi yako baada kama mara tatu kwa wiki au utakavyoamua wewe.

Kuondoa vipodozi

Mafuta ya nazi yanaweza pia kutumika kuondoa vipodozi usoni. Unashauriwa kutoa vipodozi usoni kabla ya kulala ili kuendelea kuwa na ngozi nzuri yenye afya. Chukua pamba safi chovya kwenye mafuta ya nazi kisha anza kufuta uso wako taratibu kwa kutumia pamba iliyo na mafuta ya nazi. Baada ya kufuta nawa uso wako vizuri na sabuni. Ukifanya haya utasaidia kutunza uso wako na kuwa na afya nzuri.

Kukuza nywele

Mafuta ya nazi, yanatumika katika kurutubisha nywele na kufanya ziwe na afya.

Paka mafuta ya nazi kwenye ngozi ya nywele ambazo ni hafifu au zilizokatika.

Kusaidia katika kunyoa ‘Shave oil’

Wengi wetu tumezoea kutumia krimu ya kunyoa, lakini mafuta ya nazi pia yanaweza kutumika hapa badala ya krimu hiyo. Mafuta ya nazi yenyewe yanasaidia kutibu vipele vinavyojitokeza baada ya kunyoa.

Haya mafuta wengi wanatumia katika kunyoa, yanamuacha mtumiaji akiwa laini na yanasaidia kwa kiasi kikubwa kuliko unapotumia wembe au kitu kingine.