Taifa Stars sio mboga, kocha atahadharisha
Na JOHN ASHIHUNDU
KOCHA Sebastien Migne wa Harambee Stars anaamini vijana wake wana kibarua kigumu dhidi ya Taifa Stars ya Tanzania timu hizo zitakaporudiana Jumapili kwenye pambano la CHAN.
Mfaransa huyo alisema hii inatokana na sare ya kutofungana katika mechi ya mkondo wa kwanza ugenini jijini Dar es Salaam.
Mshindi wa Jumapili atakutana na Sudan katika mikondo miwili kuwania nafasi ya kwenda Younde Cameroon mwakani kwa fainali za kombe hilo linalohusisha wachezaji wanaocheza kwenye ligi za nyumbani.
Ingawa kocha huyo anaeleza ugumu wa mechi hiyo itakayochezewa MISC, Kasarani, Wakenya wengi wanasubiri kwa hamu kuona timu yao ikiibuka na ushindi kwa vyovyote vile baada ya majuzi kushindwa kuwika katika michuano ya AFCON.
Akizungumza kuhusu mechi hiyo, nahodha wa vijana wa nyumbaji, Dennis Odhiambo alikuwa na matumaini makubwa huku akidai kwamba maandalizi ya wiki moja waliyofanya yametosha kuwapa ushindi.
Harambee Stars haijawahi kufuzu kwa fainali hizo za wachezaji wanaochezea klabu za ligi za nyumbani, hivyo, ushindi katika mechi ya Jumapili utawawezesha kusonga mbele.
Stars itakuwa ikicheza na timu ambayo inatafuta kufuzu kwa fainali hizo kwa mara ya pili, hivyo ni jukumu la kocha Migne kuhakikisha amewajenga vijana wake kisaikolojia ili watumie vyema uwanja wa nyumbani.
Timu zote zinajivunia wachezaji kadhaa waliokuwa kwenye vikosi vyao vilivyowakilisha mataifa yao katika fainali za AFCON, majuzi nchini Misri.
Hamu
Wakenya wana hamu kubwa kuona Harambee Stars ikiwa miongoni mwa timu zitakazokuwa Younde kushiriki michuano ya CHAN mwakani, kitu ambacho kitawapa mashabiki raha tele baada ya kusubiri kwa muda mrefu bila kuona timu yao ikitwaa taji lolote.
Kuteleza katika mechi ya Jumapili kutakuwa na gharama kubwa kwa kikosi kizima pamoja na idara ya kiufundi ya kocha Migne, hasa baada ya timu hiyo kubanduliwa mapema katika michuano ya AFCON.
Maelfu ya Wakenya wanatazamiwa kumiminika uwanjawa Kasarani kuwapa vijana wa nyumbani morali, hali itakayofanya mechi hii kuwa na msismko mkubwa.