Buriani Joyce Laboso
Na CAROLINE WAFULA [email protected] na VICTOR RABALLA [email protected]
WAOMBOLEZAJI Jumamosi asubuhi wamemiminika kwa wingi katika Shule ya Upili ya St Augustine Kandege, Fort Ternan, Koru, Muhoroni kwa ibada maalumu kabla kumzika Gavana wa Bomet marehemu Dkt Joyce Laboso baadaye leo.
Programu ya utaratibu wote wa mazishi imeamza saa nne kasorobo mwili wake ulipoletwa kutoka nyumbani kwake huku ukisindikizwa na familia na uongozi wa Kanisa ACK Maseno Mashariki na Dayosisi ya Kapsabet.
Rais Uhuru Kenyatta amewasili dakika chache baada ya saa sita mchana.
Naibu Rais William Ruto, aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, makamu wa Rais wa zamani Kalonzo Musyoka, kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi ni miongoni mwa viongozi ambao pia wanahudhuria mazishi katika Shule ya Upili ya St Augustine Kandege ambapo ibada inafanyika kabla ya safari ya mwisho ya kumzika Joyce.
Maiti ya gavana ilipelekwa nyumbani alikoolewa Ijumaa jioni ikitokea Bomet.
Helikopta iliyosafirisha mwili huo ilitua katika Shule ya Msingi ya St Augustine katika wadi ya Muhoroni-Koru, Kaunti ya Kisumu County.
Mumewe marehemu Dkt Edwin Abonyo, watoto na jamaa walikuwemo. Wengine walikuwa ni Naibu Gavana wa Bomet Dkt Hillary Barchok, Gavana wa Kericho Paul Chepkwony na Mwakilishi wa Wanawake wa Kisumu katika Bunge la Kitaifa Rosa Buyu.
Mbunge wa eneo hilo James Koyoo aliwapokea ambapo maombi yaliendeshwa na Askofu wa ACK Maseno Mashariki Joshua Owiti.
Wakazi walionekana wenye hamu kubwa kuutazama mwili wa mwendazake, japo hali ya usalama ilikuwa ni ya juu zaidi. Walioruhusiwa walionyesha heshima.
Mkazi mmoja alielezea masikitiko yake.
“Inasikitisha sana kuona Gavana Laboso akiwa katika jeneza. Hata hivyo, tunafurahi kuruhusiwa kuutazama mwili,” alisema mkazi Joyce Akinyi.